The House of Favourite Newspapers
gunners X

Amani ya Moyo Ni Tunu, Itunzeni Kwa Gharama Yoyote!

0

MUNGU ni mwema sana! Tunakutana Jumatatu nyingine kwenye uwanja wetu huu maridhawa, kupeana elimu ya uhusiano. Ni vyema na haki tumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini pia tuzidi kumuomba atuepushe na gonjwa hili hatari la COVID-19 linalosababishwa na Virusi vya Corona.

 

Tuzidi kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalam wa afya hususan Wizara ya Afya. Nawa mikono kila mara, epuka msongamano na safari zisizokuwa na ulazima. Kwa pamoja tunaweza kuzuia maambukizi zaidi ya gonjwa hili.

 

Turudi kwenye darasa letu, ndugu zangu, maisha ya uhusiano siku zote yanabebwa na furaha, amani na upendo wa dhati. Vinapokosekana vitu hivi, maisha ya uhusiano hayawezi kuwa sehemu salama tena. Uhusiano unageuka kuwa uwanja wa vita.

 

Panapokosekana amani, furaha na upendo wa dhati, hapo kwa vyovyote chuki hutawala. Katika hali ya kawaida, si mwanaume au mwanamke anayetamani kuishi kwenye chuki. Hakuna yeyote kati ya wawili hawa ambaye anapenda kuishi kwenye ugomvi na mafarakano, lakini kuna wakati tu mnajikuta imetokea hata kama wenyewe hamtaki.

 

Katika hali ya kawaida, kila mmoja wenu anatamani pengine kuishi kwenye raha mustarehe maisha yake yote. Lakini katika uhalisia, maisha hayapo hivyo, lazima kuna siku mtagombana. Kuna siku mtahitilafiana, mtanuniana.

 

Kuna watu wanaishi muda mrefu bila hata kuzungumza wakati ni wapenzi. Achana tu na wapenzi, kuna wengine ni wanandoa, wanaishi kwenye ugomvi kwa muda mrefu. Hakuna ambaye anakuwa tayari kujishusha.

 

Kila mmoja anajiona mjuaji. Anajiona hana kosa bali mwenye kosa ni mwenzake. Hivyo wanachagua maisha ya kukomoana. Kila mtu aishi na maisha yake. Hata kama wanaishi nyumba au chumba kimoja, kila mtu anatoka na hamsini zake.

 

Wanandoa wengi najua mtakuwa mashahidi juu ya hili ambalo ninaliandika hapa. Wapo watu wana miezi hawazungumzi, wengine mwaka na hata miaka, kila mtu anaishi bila kumsemesha mwenzake. Eti kila mtu ana mahali kwingine kwa kuifurahisha nafsi yake, ndoa inabaki tu kama jina.

 

Maisha yanaendelea wakiwa kwenye hali hiyo. Ndugu zangu, hata kama tunaona huu ni ujanja, lakini haya si maisha. Ni hatari kuishi maisha ya aina hii kwa muda mrefu. Inapotokea kwenye maisha mmeingia kwenye tatizo la namna hii, jitafakarini.

 

Kila mmoja kwa namna yake, akae chini na afikiri mara mbilimbili nini maana halisi ya ndoa au uhusiano wenu. Mliyaanza maisha ya uhusiano mkiwa na lengo gani? Penzi mlilichagua kuwa sehemu ya furaha, upendo na amani au sehemu ya vita?

 

Hakika jibu litakuwa ni kuwa mliichagua furaha. Mlikutana, mkapendana na kukubaliana kuishi kama wapenzi, marafiki, mke na mume. Kumbukeni ahadi yenu ya kwanza. Kumbukeni kwamba kuishi kwenye vita, chuki au uadui ni dhambi na hata Mungu hapendi.

 

Mjiulize, mkifa leo kwenye hali hiyo mtakwenda kujibu nini kwa muumba wenu? Chagueni maisha ya furaha, mpendane kwa dhati na hata ikitokea mmetofautiana, basi baada ya muda mfupi mnahakikisha mmeirejesha amani.

 

Kila mmoja aone ana wajibu wa kuwa furaha kwa mwenzake, amtie moyo kwenye magumu na mapito yote ya hapa duniani. Mkifurahi mnakuwa pamoja na hata kwenye matatizo pia mnaingia pamoja.

Mimi kwa leo naishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine. Unaweza kunifuata Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Erick Evarist

Leave A Reply