AMBER LULU AKIRI KUPORA MUME WA MTU
MBONA pambe! Lile sakata la mwanamuziki wa Bongo Fleva, Lulu Euggen ‘Amber Lulu’ kutembea na mume wa video vixen anayekuja kwa kasi, Haitham limechukua sura mpya baada ya sarakasi za mitandao ya kijamii kudumu kwa muda mrefu.
Kwa muda mrefu Haitham amekuwa akimtuhumu Amber Lulu kumkwapulia mumewe, madai aliyoyatoa katika mitandao ya kijamii, jambo lililosababisha warushiane maneno makali.
Cha kushangaza ni pale ambapo Amber Lulu anaibuka na kusema ni kweli anammiliki jamaa huyo wa Haitham. Akizungumza na Risasi Jumamosi, Amber Lulu ambaye anatamba na kibao chake cha‘Jini Kisirani’alisema kuwa na huyo jamaa huyo siyo stori, ila anachopaswa kujiuliza Haitham ni sababu za mumewe kumkimbia na kumfuata yeye.
“Jamani namsikitikia sana huyo Haitham, kutwa kwenye mitandao kuwa nimemchukulia mwanaume wake, hajisikii vibaya? Kwa nini mwanaume kamuacha yeye kaja kwangu? Hapo ndiyo pa kujiuliza,” alisema Amber Lulu na kuongeza: “Haitham kwa sasa ananyonyesha, ni vyema akajituliza kuliko kurusha matusi mitandaoni, haisaidii maana huyo mwanaume mwenyewe kurudi kwake ni ndoto.”
Majibu ya Amber Lulu yalimshtua mwandishi wetu, akataka kujiridhisha kama aliyosema alimaanisha, akagongea msumari wa mwisho:
“Nilichoongea ndiyo hivyo, namshauri huyo Haitham ajitathimini.” Risasi Jumamosi halikuwa na cha kuongeza, likamvutia waya Haitham ili kusikia upande wake, hakupatikana. Tunaendelea kufuatilia sakata hili kwa karibu na tutawahabarisha katika matoleo yanayofuata.
Comments are closed.