The House of Favourite Newspapers

AMCHOMA VISU MKEWE, AJIUWA


DAR ES SALAAM: Steven Mwashilindi, Mkazi wa Tabata -Kimanga jijini Dar, amedaiwa kujiua baada ya kumchoma visu tumboni mkewe, Maida Julius kisha na yeye kujichoma kisu na hatimaye kujimalizia kwa kujinyonga hadi kufa.

TUMSIKILIZE MDOGO WA MAREHEMU

Akizungumzia tukio hilo la kutisha, mdogo wa marehemu, Wema Mwashilindi, alisema lilitokea usiku wa Oktoba 13, mwaka huu. Alisema siku ya tukio, alipigiwa simu na majirani wa marehemu ambao walimfahamisha kuhusu tukio hilo.

“Nilipigiwa simu na majirani wakaniambia kuwa kaka yangu amefariki dunia kwa kujinyonga baada ya kumchoma visu mkewe, ikabidi niende eneo la tukio nijue kulikoni mpaka akaamua kuchukua uamuzi mzito namna hiyo,” alisema mdogo huyo wa marehemu.

Aliongeza kuwa alipofika, alikuta kweli tukio hilo limetokea na kwamba majirani wanafanya jitihada za kumuwahisha mke wa marehemu hospitali kwani alikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake huku akivuja damu nyingi

MJOMBA ALISHUHUDIA

Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mjomba wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Frank, alisema kuwa marehemu alijiua kutokana na kudhani kuwa ameshamuua mke wake.

“Ilikuwa siku ya Jumamosi usiku mida ya saa mbili hivi usiku, marehemu na mke wake walikuwa wanagombana ndani baada ya hapo mkewe alipiga kelele ndipo tulipoingia ndani na kuwakuta wamelaliana wakipigana huku mke wa marehemu akiwa na majeraha ya visu.

 

“Ikabidi tuwaachanishe, tukamchukua mgonjwa tumuwahishe Hospitali ya Tabata pale tukaambiwa tumpeleke Hospitali ya Amana na tulipofika Amana, tukaambiwa tumpeleke Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na tulipomfikisha, akalazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji huduma maalum (ICU) kwa sababu utumbo ulikuwa nje,” alisema mjomba na kuongeza:

“Kumbe huku nyuma marehemu aliingia chumbani nafikiri alijua kuwa ameua, akachukua kisu na kujichoma, alipoona anachelewa kufa akachukua kamba na kujinyonga hadi kufa kwani tuliporudi hospitali tulimkuta ananing’inia, amejinyonga chumbani kwake.”

HISTORIA YA MAREHEMU

Akizungumzia historia ya wawili hao, mdogo wa marehemu, Wema alisema kaka yake na mkewe walikuwa na ugomvi mdogo kabla ya kutokea kwa tukio hilo.

 

“Ninavyokumbuka ni kwamba marehemu alikuwa na ugomvi (hakuutaja ni ugomvi gani) na mke wake ingawa haukuwa mkubwa sana ambapo mkewe aliamua kwenda kwa mjomba yake wiki mbili zilizopita, sasa akiwa kule alipigiwa simu kwamba mume wake anataka kuhama bila kumpa taarifa kwa hiyo akasema watoto itakuwaje?

 

Ndipo alipoamua kuchukua uamuzi wa kurudi ili awaangalie watoto na ndipo ulipotokea ugomvi hadi kutokea hayo yaliyotokea,” alisema Wema.

Kwa upande mwingine, mjomba wa marehemu, Frank alidai kuwa, marehemu alifikia hatua hiyo baada ya kuhisi kuwa mwenye nyumba waliyokuwa wanaishi na mkewe wamefanya njama ili wamtoe kwenye nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi kwa kuwa walikuwa wanadaiwa kodi.

Hadi tunakwenda mitamboni, ndugu hao walisema mke wa marehemu alikuwa amehamishiwa katika wodi ya kawaida katika Hospitali ya Muhimbili na kwamba hali yake inaendelea vizuri. Mwili wa marehemu uliagwa juzi Jumanne katika Hospitali ya Amana jijini Dar na kusafirishwa kuelekea mkoani Songwe kwa ajili ya mazishi.

 

Enzi za uhai wake marehemu alikuwa mwanachama wa Simba Tawi la Tabata-Kimanga. Ameacha mjane mmoja na watoto watatu. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamdan alipotafutwa kuhusiana na tukio hilo alisema yupo nje kiofisi na taarifa hizo hazijamfikia.

Waandishi: Memorise Richard na Neema Adrian.

Comments are closed.