Ame Ally Azuiwa Singida

MCHEZAJI mpya aliyesajiliwa na Singida United, Ame Ally, amezuiwa kuitumikia klabu hiyo na Bodi ya Ligi ili kupisha uhakiki wa uhalali wa usajili wake.

 

Mchezaji huyo ambaye amewahi kuitumikia Azam FC, amezuiwa na Bodi ya Ligi baada ya kuonekana kwamba bado kuna mambo hayajakaa sawa kati yake na waajiri wake wa zamani, Ndanda.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Msemaji wa Singida, Cales Katemana, amesema bado wanasubiri taarifa rasmi kutoka Bodi ya Ligi kabla ya kuanza kumtumia.

 

“Tumekamilisha usajili wetu kwa asilimia tisini na wachezaji wote wameshaanza kucheza isipokuwa mmoja tu ambaye ni Ame Ally ambaye bado hajapata ruhusa kutoka Bodi ya Ligi baada ya kuonekana kuwa kuna mambo hayajawekwa sawa kati yake na waajiri wake wa zamani,” alisema Katemana.

 

Singida ambao juzi walijinasua mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Ruvu Shooting na kufikisha alama 10, huku wakiwa tayari wameshacheza michezo 16 mpaka sasa wakishinda miwili, wamefungwa katika michezo kumi na kutoka sare minne.

 

JOEL THOMAS, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment