The House of Favourite Newspapers

Amigo: Mke Wangu Hapendi Kazi Yangu!

 

NA IMELDA MTEMA | RISASI JUMAMOSI | MPAKA HOME

NI siku nyingine, mahali petu pakujidai ni hapa ambapo tunaweza kujua maisha nyuma ya pazia ya mastaa wetu mbalimbali  Bongo, kwa kutinga majumbani mwao na kuyaweka wazi maisha yao.

Wiki hii safu hii ilipiga hodi nyumbani kwa muimbaji mahiri wa Bendi ya Jahazi Modern Taarab, Abubakary Soud ‘Amigo’ anayeishi maeneo ya  Kimara-Stop Over jijini Dar.

Mwanamuziki huyu amefungukia maisha yake halisi ya kila siku, kuyajua mengi zaidi twende pamoja chini:

MPAKA HOME: MAISHA YAKO HALISI HAPA NYUMBANI YAKOJE?

“Ni ya kawaida sana na siyo kwamba mimi ni staa najulikana sehemu nyingi nishindwe kufuata utaratibu wa mwanadamu anavyotakiwa kuishi, nafanya kila kitu ambacho watu wengine wanafanya na ninapenda sana watu na siyo mtu wa maringo kama wafanyavyo mastaa wengine.”

MPAKA HOME: VIPI KUHUSU FAMILIA, UMEOA AU UNA WATOTO TU?

“Nina mke na tuna watoto wanne sema tu kwa bahati mbaya mama watoto hujamkuta kwa sababu kaenda kwenye shughuli zake lakini bahati nzuri umewakuta hawa watoto wangu wawili, Othuman na Mwanaisha wengine wako kwa bibi yao.”

MPAKA HOME: KAZI ZAKO MARA NYINGI UNARUDI USIKU, VIPI MKEO HALETI USUMBUFU?

“Unajua hakuna mwanamke ambaye hapendi kulala na mumewe mpaka asubuhi lakini kutokana na kazi yangu inabidi kukubali maana kuna kipindi alishawahi kuniambia kwa nini nisitafute kazi nyingine kuliko ya kujitesa usiku lakini ukweli ni kwamba kazi ninayoifanya iko kwenye damu.”

MPAKA HOME: UNAPENDA KUFANYA NINI UNAPOKUWA NYUMBANI?

“Napenda kuangalia tamthiliya. Naweza nikashinda ndani kuanzia asubuhi mpaka usiku naziangalia, hiyo ndiyo hobi yangu.”

MPAKA HOME: VIPI JIKONI HUWA UNAINGIA KUMSAIDIA MKEO?

“Jamani kama kuna vitu siwezi kufanya ni kuhusu mambo ya jikoni, nilishawahi kujaribu hata kupika mayai nilishindwa hivyo ‘waifu’ namsaidia labda kufua nguo kidogo lakini jikoni hapana.”

MPAKA HOME: NI KITU GANI KINAKUKERA SANA MAISHANI?

“Kitu kinachonipa shida ni kukosa usingizi mpaka natamani kama kuna wataalamu wanisaidie maana ni tatizo sugu halafu linaniumiza sana,  kila nikijitahidi niutafute usingizi siupati kabisa, hiyo ndiyo kero yangu kwani wenzangu wanapokuwa wamelala fofofo mimi huwa nakodoa macho tu!”

MPAKA HOME: VIPI HUTAMANI WANAO WARITHI KAZI UNAYOIFANYA?

“Hapana kwa kweli sitamani hata kidogo, najipinda tu wasome shule nzuri wapate elimu ili waweze kufanya kazi nyingine siyo kama hii labda warithi ucheshi wangu na nyota yangu ya kupendwa na watu.”

MPAKA HOME: MUZIKI UNA MAMBO MENGI HUSUSAN USIKU MNAPOKUWA KWENYE KUMBI, VIPI KUHUSU VISHAWISHI VYA WANAWAKE?

“Hivyo vipo vingi lakini kwa sababu najitambua na tayari nimeoa huko nje hakuna jipya, mambo ni yaleyale.”

MPAKA HOME: MPANGILIO WAKO WA CHAKULA UKOJE KILA SIKU?

“Nikiamka jambo la kwanza kabla ya kupiga mswaki lazima ninywe maji mengi ili kutengeneza sauti halafu nipate mayai ya kukaanga na kuhusu mchana nakula chakula chochote.”

MPAKA HOME: KITU GANI UNAKITAMANI NYUMBANI KWAKO KIWEPO? “Nilitamani kuwe na banda la kuku ningefurahi sana maana mimi napenda sana ufugaji na hata kulimalima kwa sababu hata nje kwangu nimepanda matunda kama mapasheni.”

Comments are closed.