The House of Favourite Newspapers

Amina Chifupa Akumbushia Vita ya Madawa ya Kulevya

0
Marehemu Amina Chifupa enzi za uhai wake.

HOW To Get Rich (Jinsi ya kuwa tajiri), ndiyo jina la kitabu nilichokuwa nimekishika mkono wa kushoto, ambacho mwandishi wake ni Rais wa 45 wa Marekani, mfanyabiashara maarufu, Donald Trump.

 

Manyunyu ya mvua yakiishia kwa mbali huku nikikanyaga kwa kunyata taratibu, niko mahali ambako sipajui. Juu hakuna mawingu wala jua achilia mbali nyota, lakini kuna mwanga mweupe ambao kwa hapa nashindwa kueleza kwa maandishi, hata kwa mdomo siwezi. Naangalia pembeni hakuna ukuta, ni sehemu yenye kutisha.

 

Sauti za vilio vya vyura madimbwini, vinayapa tabu masikio ingawa sioni dalili yoyote ya maji, zaidi ya yale matone ya mvua. Wakati nashangaa mazingira hayo, ghafla nafunikwa macho kwa viganja. Ni ulaini na manukato ya viganja hivyo vinanifanya nigundue ni vya mwanamke.

 

Hata hivyo ananiachia na kuja mbele yangu, tunatazamana na hapo ndipo nakutana na sura ya kuvutia, Amina Hamis Chifupa! Haraka sana natoa kitabu cha kutunzia kumbukumbu (notebook) na kalamu, tayari kwa mahojiano na nimeshasahau kabisa ugeni wa mazingira hayo. Fuatana nami katika mahojiano haya maalum na marehemu Amina Chifupa. Mimi: Waoh, habari za siku? Amina: Salama sana, karibu huku kwetu tumeshapazoea. Mimi: Asante, unajisikiaje kuwa huku mwenyewe na upweke huu?

 

Amina: Upweke? Siko mwenyewe, juzi tu nimempokea baba yangu, yuko mtaa wa pili kutoka hapa lakini pia majirani zangu ni akina Chacha Wangwe, pale panapowaka mwanga mkali wa umeme ni kwa Mtikila na kule nyuma kwenye ile miti ni kwa Salome Mbatia, hivyo tuko wengi (anaendelea)… Baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake nani amemrithi? Mimi: (natabasamu kidogo), Ni Dk. John Pombe Joseph Magufuli, kwa sasa ni kazi tu. Nchi imetulia na hakuna tena ufisadi mambo ya wizi wa mali za umma, wanatumbuliwa ile mbaya. Amina: Safi sana hata mimi nilikuwa namkubali sana.

 

Lowassa na Sumaye hawakugombea tena? Vipi kuhusu Prof. Mark Mwandosya na Salim Ahmed Salim? Mimi: Wapo lakini Sumaye na Lowassa wameshahama chama na sasa wako Chadema na Lowassa aligombea nafasi ya urais kupitia Chadema, ndiye alikuwa akishindana na Rais Dk. Magufuli.

 

Amina: (akijifunika mdomo kwa viganja na kisha kuachama) unasema kweli Masalu? Mambo yamebadilika sana. Vipi, kipindi cha Leo Tena pale Clouds nani anakiendesha sasa hivi?

 

Mimi: Ni wengi wamepita tangu wewe uondoke lakini kati yao ni Dina Marious na Gea Habibu, kinafanya vizuri

 

Amina: Vipi, Global bado mnaendelea na habari za kufichua maovu? Mimi: (haraka sana) tena ndiyo kwanza kumekucha, siku hizi tuna TV ya mtandaoni inaitwa Global TV Online, inaongoza kwa habari mbalimbali za kijamii, mastaa na michezo, umepitwa na mengi sana.

 

Amina: Dah! Kweli kabisa. Hivi tangu niondoke huko kuna mwanasiasa yeyote alishavaa ujasiri wa kuanika wauza dawa za kulevya kama ambavyo nilikuwa nimedhamiria kutaja orodha yao?

 

Mimi: (nikijiweka sawa kumjinu vyema), yupo mmoja tu. Tena yeye ni fundi kwelikweli, aliwataja hadharani watuhumiwa na kuwataka wajisalimishe wenyewe. Anaitwa Paul Makonda, ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Amina: Simfahamu, lakini amefanya vyema sana. Hata mimi nilipanga nifanye hivyo basi tu Mungu aliniita ghafla. Enhe, nimekumbuka ile kesi ya Manji na Mengi ya kudaiana shilingi moja ilifikia wapi? Mimi: Ilishaisha na maisha yanasonga kwa upendo kabisa.

 

Amina: Vipi, kuna wabunge gani vijana wanaotetea maslahi ya taifa kama ilivyokuwa kwangu? Mimi: Wapo wengi tu. Akina Nape Nnauye, Hussein Bashe, Joshua Nasari na wengine siku hizi ni mawaziri kama Juliana Shonza na wengine wengi. Amina: Siku za hivi karibuni umeshatembelea nyumbani kwetu? Ulimkuta mwanangu Abdulrahman? Anaendeleaje na masomo? Gari langu ulilikuta?

 

Mimi: Tena umenikumbusha. Mwanao bwana ni mjanja sana. Kuna siku tulienda kufanya naye mahojiano. Kamera yetu ikawa na tatizo la lensi, akapiga picha kupitia simu yake kwa ahadi ya kuturushia baadaye, hakufanya hivyo bwana. Tulikuta magari kama matatu likiwemo hilo ulilokuwa unalitumia. Amina: Namjua mwanangu, alikuwa mtundu tangu mdogo, poleni lakini ni utoto tu, tena baba yake huyo anakuja.

 

Vipi, Zitto Kabwe yupo? Ameshaoa? Bado anaendelea na siasa zake za ujasiri? Mimi: Yupo na ana mke. Siku hizi ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACTWazalendo, alishaachana na Chadema. Amina: Duh! Mbona kuna mapya mengi sana huko jamani! Sasa, leo kuna sherehe kwa Regia Mtema, si unamkumbuka? Kuna tafrija fulani kwa hiyo kwa heri wenzangu akina John Komba, Cellina Kombani, Jeremiah Sumari na mzee Samuel Sitta, ambao tuko kwenye kamati ya maandalizi wananingoja. Mimi: Sawa Amina, wasalimie. Lakini hapa ni wapi? Mbona sipaelewi kabisa? Amina: Siwezi kukwambia ni wapi lakini ni eneo tulivu lisilokuwa na karaha kabisa, wasalimie huko. Msalimie sana Ruge (Mtahaba) na Shigongo (Eric), bila kumsahau Zitto ukimuona. Mimi: Sawa Amina lakini umependeza na hata mwili wako umeongezeka. Amina: (Kicheko tu na kisha kunipungia mkono) Hapohapo nami najiandaa kuondoka lakini ghafla nashtuliwa na mwanga wa jua la asubuhi. Ayaaa kumbe nilikuwa naota bwana, bahati nzuri ilikuwa siku ya Jumamosi, siku ambayo sina majukumu ya kazi, nikajilaza na kuusaka tena usingizi lakini sikuota chochote.

Makala: Brighton Masalu.

VIDEO: Sauti ya Tundu Lissu Alichokisema Baada ya Kutoka ICU!

Leave A Reply