The House of Favourite Newspapers

Amini Afungukia Watu Kupenda Mahusiano Yake Na Linah

0

AMINI Mwinyi Mkuu ndiyo jina halisi alilopewa na wazazi wake, lakini kwa mashabiki wa Bongo Fleva hapa nchini wanamjua kwa jina moja la Amini.Kijana huyu ni miongoni mwa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva waliotokea kwenye nyumba ya vipaji Tanzania House of Talent (THT).

 

Amini ni moja kati ya wasanii waliopata umaarufu mkubwa kutokana na kazi yake ya sanaa, kama unakijua kibao cha Robo Saa, basi tambua kuwa ni ubunifu wa Amani, mpe tu heshima yake.

 

Hivi Karibuni Amani lilifanya mahojiano na Amini ambapo amefunguka mambo mengi, kubwa zaidi ni kuhusiana na habari zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya kwamba amerudiana na aliyekuwa mpenzi wake wa zamani Linah Sanga “Linah” na kusababisha ndoa yake kuvunjika.

AMANI: Kwanza hongera kwa wimbo wako mpya wa Vaga Vaga, unazungumziaje mapokeo yake?Amini: Mapokezi ya Vaga Vaga siyo mazuri sana wala siyo mabaya sana, ila ni wimbo ambao niliutoa kama bonus tu kwa mashabiki wangu, haukua official, lakini asilimia kubwa wengi wameupenda na wanatamani kuona video yake itakuwaje, nashukuru Mungu kwa hilo.

 

AMANI: Kwa upande wako, Corona imekuathiri vipi kwenye mambo yako ya muziki?

 

Amini: Corona siyo kwangu tu, ni kwa wasanii wote kwa sababu shoo zimezuiwa kutokana na katazo la mikusanyiko na wasanii wengi tulikuwa tunaandaa shoo kwenye mikoa tofauti, lakini kwa sasa hivi hatuna mamlaka yoyote ya kufanya hivyo kutokana na janga hili, hata kazi pia nazo hazisambai kivile kama ilivyokuwa hapo awali, nyimbo nyingi zinabuma.

 

AMANI: Kama ulivyosema sasa hivi msanii akitoa nyimbo zina buma na pesa hakuna kwa sababu mlikuwa mnategemea shoo kupata kipato, je, kwa upande wako una biashara yoyote ambayo unaifanya ili iweze kukuingizia kipato kwa kipindi hiki cha janga hili la Corona?

AMINI: Biashara zipo, ila siwezi kuzianika.

 

AMANI: Kwa kipindi hiki cha janga la Corona, wasanii wengi watapoteza mashabiki kutokana na kutoa nyimbo halafu hazihiti kama hapo awali, kwa upande wako ni njia gani utatumia kuhakikisha haupotezi mashabiki wako?

AMINI: Kwanza kabisa kuna mitandao ya kijamii, watu wengi wanatembelea huko, kwa hiyo mimi kama Amini muda mwingi napenda kuchukua gitaa langu, napiga ala na kuziweka kwenye status yangu na mashabiki wangu wanaona kuwa Amini yupo na pia naposti vitu kwenye Instagram.

 

AMANI: Unalidhika na hicho unachowafanyia mashabiki wako?

 

AMINI: Kabisa naamini kwa kufanya hivyo nakuwa karibu nao kwa sababu nawatengenezea mazingira ya kwamba waendelee kuona kwamba bado nipo na ninafanya kazi na pia nina ‘share link’ kwenye magroup kupitia namba zangu za simu mashabiki waendee You Tube kwa sababu hata huko kuna pesa na platifomu ya mashabiki.

 

AMANI: Wasanii wengi wamekuwa na mtindo wa kutoa EP au Albam fupi, je kwa upande wako suala hili limekaaje?

 

AMINI: Plani ya kutoa EP ipo lakini kuna upepo fulani nausubiri upite kidogo halafu ndiyo nitoe.

 

AMANI: Kwa nini isiwe sasa hivi?

 

AMINI: Kumbuka kuwa mimi ni mwanamuziki ambaye nyimbo zangu ni kusikiliza, siyo nyimbo za kukurupuka tu, mimi nina aina ya mashabiki ambao wanaoupenda muziki wangu, sipendi kukurupuka ngoja mambo yawe sawa nitatoka.

AMANI: Sasa hivi ukiangalia muziki umekuwa kwenye ushindani mkubwa sana tofauti na ule wa zamani, labda kwa upande wako una kipi cha tofauti ili kuhakikisha haushuki kimuziki?

 

AMINI: Kwanza mimi naishi katika misingi ya mwamuziki, mimi siyo msanii bali ni mwanamuziki, napiga gitaa na kuimba pia naweza kupiga Live Band na kipaji hiki unachokiona kimepikwa pia darasani, nimefundishwa misingi ya kuwa mwanamuziki bora kwani ni lazima kuiheshimu kazi yako, kuamini kile kitu unachokifanya na kutokutaka mashindano na mtu wa aina yoyote, bali kufanya kile ulichojaaliwa, mbinu hii ndiyo naitumia kwenye sanaa yangu ndiyo maana watu wanamuona Amini yupo na hatetereki.

 

AMANI: Changamoto unazozipitia kwenye mambo yako ya muziki ni zipi?

 

AMINI: Kusema kweli kama una kipaji huwezi kuziona changamoto katika suala la muziki, ila changamoto kubwa kwa sasa ni kwamba muziki unahitaji fedha nyingi, na pesa imekimbia na mwanamuziki unatakiwa kushuti video katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi na unaweza ukatumia hata milioni 7 kutengeneza video lakini ukija kutoa wimbo, unashindwa kukurudishia gharama uliyotumia.

 

AMANI: Mafanikio gani ambayo unajivunia kwenye muziki wako?

 

AMINI: Mafanikio yako mengi, lakini moja ni kufanikiwa kufikisha ujumbe kwenye jamii kupitia sanaa yangu.Kingine ni kwamba, najivunia kusaidiana na watu wengine kwa sababu kuna wanamuziki wenzangu wengi nimewasaidia kimawazo na hata kuwaandikia nyimbo.

 

AMANI: Ni akina nani hao?

 

AMINI: Mwasiti nilimuandikia wimbo uitwao Mapito, Linah nilimwandikia Bora Nikimbie, Peter Msechu nilimuandikia wimbo wa Nyota.

 

AMANI: Mitandaoni kuna ishu hoti sana kuhusu wewe na Linah, inasemekana umerudiana naye na ndiye amesababisha hata kuvunjika kwa ndoa yako, je jambo hili lina ukweli wowote?

 

AMINI: Siyo kweli, uhusiano wangu na Linah ni wa zamani nafikiri ulikuwa unawafurahisha wengi ndiyo maana hata sasa wanatamani kutuona tuko pamoja, ndiyo maana wanatuunganisha hata kama tumeachana.

 

AMANI: Neno la mwisho kwa mashabiki wako.Amini: Kikubwa wapende muziki mzuri, kilicho bora na wasiache kusapoti wasanii hasa wachanga ambao wana ndoto ya kuwa kama Amini; kingine tuendelee kujikinga na gonjwa hili la Corona

MAKALA: KHADIJA BAKARI

Leave A Reply