The House of Favourite Newspapers

Amkimbia mama mkwe, kisa kukeketwa!

AMANI (4)Veronica Antony

VERONICA Antony (22), mkazi wa Mwanza amelazimika kutoroka kwa wakwe zake, Musoma, Mara kwa sababu ya kulazimishwa kukeketwa na kuolewa na shemeji yake baada ya mumewe kufariki dunia.

AMANI-(2)Veronica akiwa na mwanaye aliyeungua mkono.AMANI-(3)Veronica akiwa na watoto wake wawili

Akizungumza na Amani hivi karibuni, Veronica alisema mwaka 2012 akiwa Mwanza alipokuwa akiishi na mama yake mzazi, Sophia Ruben aliolewa na Antony mwenyeji wa Musoma, lakini mapema mwaka jana mumewe huyo alifariki dunia kwa ajali ya bodaboda.

“Mume wangu alipofariki aliniachia mtoto wa miaka miwili (Ruben) huku nikiwa na mimba ya miezi minne. Wakati huo mama alikuwa amehama Mwanza na kwenda Chanika (Dar) hivyo nikalazimika kwenda Musoma kuishi kwa wakwe zangu,” alisema Veronica.

Aliongeza kuwa, baada ya kujifungua mtoto (Gladness), machafuko ya familia yakaanza ambapo mama mkwe wake, alimtaka aolewe na shemeji yake aitwaye Agustino ambaye ana mke na watoto watatu.

“Lakini aliniambia siwezi kuolewa bila kukeketwa kwa kuwa ndiyo mila za kwao jambo ambalo marehemu mume wangu alipingana nalo kipindi ananioa. Nikalazimika kumweleza mama yangu kwa njia ya simu, akaniita Dar.

“Jumatano ya wiki iliyopita (Novemba 25 mwaka huu) kabla sijaja Dar, mkwe wangu huyo aliniambia nikasuke, shughuli ya kukeketwa ipo tayari. Ndipo usiku wa siku hiyo nikatoroka na watoto. Lakini tukiwa safarini kuja Dar, majambazi walituvamia nikaibiwa simu niliyokuwa nikiwasiliana na mama,” alisema Veronica.

Kufuatia tukio hilo la kuibiwa simu, Veronica alipoteza mwelekeo kwa kuwa hajui atampataje mama yake. Kwa sasa amehifadhiwa Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar akiwa na watoto wake wawili ambapo mmoja wapo aliungua na uji siku chache kabla ya kusafiri. Ameandikiwa jalada namba OB/RB/18899/2015 TAARIFA.

Mkwe wake alipotafutwa na polisi alikataa kutoa ushirikiano kwa kudai ameingizwa hasara kubwa ya kuandaa shughuli hiyo ya kukeketwa.

Comments are closed.