The House of Favourite Newspapers

Amua Yaliyopita Si Ndwele, Ganga Yajayo

0

NI Ijumaa nyingine njema, tunamshukuru Mungu kwa kutujaalia kuiona siku hii pamoja na kwamba, tunapita kwenye changamoto nyingi.

Rafiki zangu, watu wakiachwa na wachumba wao au wakipigwa talaka, huanza maisha mapya ya mapenzi. Wataalam wanasema watu hao huwa na kipindi kigumu baada ya kuachwa na kabla ya kupata wachumba wapya.

 

Wanasema kuachwa na mpenzi au kupewa talaka kunasononesha hata kwa wale ambao hupeana talaka wenyewe.

Haijalishi ni nani anayeacha mwenzake, anayeachwa au sababu ya kuachana.

Ukweli ni kwamba, talaka au kuachwa humuathiri mtu na maisha yake kwa ujumla.

 

Wanaojikuta kwenye hali hii huogopa kujihusisha tena na mapenzi.

Japokuwa inategemea sababu na mazingira ya kuachana, watu wengi huchelea kuanza maisha mapya ya mapenzi. Hata hivyo, kuna mbinu na hatua za kufuata ili kuhakikisha mtu anafurahia maisha hata kama ameachwa.

Watu wengi huwa wanaalika sononeko kwa kunyamaza na kujitenga na watu wengine bila kufahamu kwamba kuzungumzia masahibu yao ni tiba.

 

Badala ya kunyamaza na kusononeka peke yako, mtafute mtu unayemwamini umfungulie moyo wako. Anaweza kuwa jamaa yako wa karibu, rafiki au mchungaji wako. Hakikisha unayemfungulia moyo wako ni mtu ambaye hatatumia masahibu yako kukuvunja moyo zaidi au kukutumia vibaya.

 

Katika hali kama hii, yafaa utafute msaada kutoka kwa washauri nasaha waliobobea kama sisi waandishi wa makala hizi, tutakuponya wewe na uhusiano wako.

Kwa kuogopa upweke, watu wengi huwa wanaangukia mitego ya walaghai wa mapenzi kwa kusaka wapenzi wapya kwa pupa.

 

Ukiwa katika hali kama hii, yakupasa kuchukua muda kabla ya kuanza uhusiano mpya wa mapenzi. Kuchukua muda kutakusaidia kuelewa kilichovuruga uhusiano wako wa nyuma. Muda huo unakufanya utulie na kufanya uamuzi unaofaa.

Ni makosa makubwa kujitosa kwenye uhusiano mpya wa mapenzi kwa sababu ya hasira ya kuachwa.

Kwa kawaida hasira ni hasara na itakuongezea mateso zaidi moyoni.

 

Kuna wanaojibwaga kwenye uhusiano mpya wakidai wanataka kulipiza kisasi kwa kuachwa na wachumba wao. Kuingia kwenye uhusiano wa mapenzi kwa sababu ya hasira au kulipiza kisasi ni hatari mno.

Watu wengi hufanya makosa kwa kuanza uhusiano mpya ili kujituliza badala ya kufanya lililo sahihi kuponya roho zao baada ya kupigwa teke na wapenzi wao.

 

Acha yaliyopita yasiwe ndwele kwako, amua kuganga yajayo. Tulia usije ukatumbukia mikononi mwa watu wabaya tena kwa sababu ya kufanya uamuzi usiofaa. Kilicho muhimu kwako siyo kuondoa upweke, ni kupata mtu ambaye atakupa maisha ya raha. Lakini kumbuka maisha ya raha huanza na mtu binafsi.

 

Huwa ninakumbusha watu kuwa kuanza uhusiano wa mapenzi baada ya kuachwa siyo rahisi na mtu huwa anahitaji watu kumtia motisha na kumchochea kurejea kwenye maisha ya mapenzi.

Hata hivyo, huwa inategemea watu ambao mtu huamua kuwa karibu nao.

 

Mtu akiachwa, si sahihi kufananisha watu wengine na mpenzi wake wa zamani.

Tarajia kwamba, mpenzi wako mpya atakuwa tofauti kabisa na aliyetangulia.

Usifananishe wapenzi wote utakaokutana nao na mpenzi wako wa zamani.

 

Muhimu ni kuvutiwa na tabia ya mtu. Hiki ndicho kigezo muhimu kwa uhusiano wa mapenzi wa muda mrefu.

Watu wanaosaka wapenzi wapya baada ya kuachwa, hujikuta wakitoa miili yao kutumika ovyo wakiamini wamepata mbadala, matokeo yake hujikuta wakilia tena na tena kwa kutendwa vibaya. Kufanya hivi si kwamba tu utaishia kuchezewa, lakini humuongezea mtu sononeko maradufu.

 

Hata hivyo, hali hii haifai kuwa sababu ya kujinyima raha ya penzi utakapobahatika kupata mtu mwaminifu.

Kwa leo naishia hapa, nakutakia kila la heri kwenye penzi lako, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine bomba.

 

Hashim Aziz

+255 719401968

 

Leave A Reply