The House of Favourite Newspapers

Amuua Mkewe Kinyama Akidai Penzi!

0

VILIO na simanzi, imetanda katika kitongoji cha Kwihuri kilichopo Kijiji cha Buturu, kata ya Butiama, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, baada ya mkazi mmoja wa kitongoji hicho, Amosi Joseph Wagunya (37) kumuua kinyama mkewe Esta Masunga (33) kwa kumpondaponda kichwani kwa kutumia pondeo la mihogo, kisha kujiua kwa kunywa sumu.

 

Aidha, chanzo cha mauaji hayo, kimeelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi baina yao, ambao ulisababisha mgogoro ndani ya ndoa yao, uliodumu zaidi ya miaka miwili.

 

TUKIO LILIVYOKUWA

Akizungumzia tukio hilo la kikatili lililojiri muda wa saa tatu asubuhi Septemba 10 mwaka huu nyumbani kwa wanandoa hao, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Buturu, Joseph Maregesi alisema chanzo cha tukio hilo, ni wivu wa kimapenzi.

Mtendaji huyo alisema Wagunya alikuwa akilalamika kuwa, mara kadhaa amemkuta mkewe na wanaume wengine, kitendo ambacho kilisababisha mkewe kumnyima unyumba kwa zaidi ya miaka miwili.

 

Alisema, walimhoji mtoto  huyo wa marehemu ambaye ni miongoni mwa watoto watano walioachwa yatima na kufafanua kwamba, baada ya mama yao kuingia ndani, baba yao alitoka shambani na kumshika mama yao, kisha akachukua pondeo la mihogo na kuanza kumpondaponda nalo kichwani.

 

Mtendaji huyo alisema, mtoto huyo aliendelea kuwasimulia kuwa, baada ya baba yao kumponda kichwani mama yao, alichukua kisu na kumchomachoma machoni, kisha akachukua sumu ya kuulia wadudu aliyokuwa ameitunza ndani na kunywa nusu lita.

 

POLISI WATHIBITISHA

Aidha, Kamanda wa polisi mkoani Mara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi; Daniel Shilla, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaonya wananchi kuacha kuua au kujiua  kwa kisingizio cha wivu wa kimapenzi. Alisema matukio ya aina hiyo, wanaoathirika zaidi ni wale watoto wanaokuwa wameachwa.

 

Aidha, Balozi wa shina namba tatu katika kitongoji hicho cha Kwihuri, Idd Juma Nyamazanzare, ambaye pia ni mwanafamilia katika familia hiyo, alisema siku hiyo ya tukio, Wagunya alimuita aende nyumbani kwake.

 

Alisema baada ya kuonana naye, alimtaka aorodheshe vitu vyake vyote alivyokuwa amevitunza kwa majirani, yakiwemo mabati na mbao na baada ya kuandika vitu hivyo, alimtaka balozi huyo aende na daftari hilo nyumbani kwake akalitunze. “Baada ya kurejea kwangu, ilipotimu muda wa saa 3 asubuhi, nilipata taarifa za tukio hilo la mauaji,” alisema.

 

MAMA AFUNGUKA

Mama mzazi wa marehemu Wagunya; Anastazia Wagunya, ameeleza kwamba, kutokana na mgogoro huo na majibu mabaya ya mwanamke huyo, Wagunya alichukua hatua kadhaa za kutaka suluhu bila mafanikio.

 

“Kwanza alimrudisha mkewe nyumbani kwao mara saba, lakini wazazi wa upande wa mwanamke walishindwa kumkemea binti yao na kuendelea kumlaumu Wagunya kwa kumfuatafuata mtoto wao, jambo ambalo lilizidi kumtia kiburi mwanamke huyo aliyedaiwa kumdharau mume, hivyo mume akaona ni bora amuue na yeye ajiue kuliko kupata maudhi ya mke,” alisema.

AOMBA MSAADA

Aidha, mama huyo, aliomba wasamaria wema wamsaidie fedha za kujikimu kutokana na mahitaji ya watoto hao watano walioachwa na wazazi wao baada ya kutokea mauaji hayo.

 

“Kwa sababu hali yangu kimaisha ni ngumu, familia hii ni kubwa aliyoniachia, na watoto wamebaki yatima, sijui pa kuanzia, ndiyo maana nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie chochote hata kama ni nguo au chakula, niweze kuwahudumia hawa watoto,” alisema mama huyo na kutaja namba yake kuwa ni 0769 668530.

 

STORI GREGORY NYANKAIRA, MARA

Leave A Reply