The House of Favourite Newspapers

ANAKUTESA KWA KUKOSA UAMINIFU? FANYA HAYA KUMDHIBITI

NIMEWAHI kueleza hapa kwamba hakuna kinachoumiza moyo kama kuishi na mpenzi asiye mwaminifu na leo nasisitiza, kama kweli unampenda hebu kuwa mwaminifu kwa sababu maumivu ya kusalitiwa huwa ni makali sana.  

 

Kuna wakati inatokea, unampenda sana mtu fulani na yeye ndiyo kila kitu kwenye moyo wako, lakini kila mara anakusaliti na kukutesa moyo wako. Unapokuwa kwenye uhusiano wa namna hii, ni rahisi sana kufikiria uamuzi wa kuachana naye na kuendelea na maisha yako.

 

Hata hivyo, jambo wasilolijua wengi, hakuna kazi ngumu kama kuamua kuachana na mtu ambaye bado moyo wako unampenda! Mtu ambaye mmeshaishi pamoja na kujenga historia katika maisha yenu. Japokuwa hata maandiko matakatifu yanaeleza wazi kwamba hukumu ya mtu asiye mwaminifu, ni kuachana naye!

 

Hata kama mlikuwa mmefunga ndoa yenye baraka zote za Mungu, mtu akiwa msaliti, maandiko yanatoa nafasi ya uhusiano wa namna hiyo kuvunjika, hasa kama tayari mmeshapitia hatua kadhaa za usuluhishi bila mafanikio.

 

Sipingani na maandiko hayo, lakini wakati mwingine, unakuta tayari mmeshajenga familia pamoja, mmezaa watoto na kufanya vitu vingi pamoja! Je, hata katika hatua kama hii njia pekee ni kuachana? Ukimuomba mtu yeyote ushauri kuhusu mume, mke au mpenzi anayekusaliti, majibu yatakuwa mepesi tu, hakufai huyo, achana naye.

 

Hata hivyo, hatua ya kuachana binafsi huwa ninaiona kama inatakiwa kuwa hatua ya mwisho kabisa, zipo mbinu za kushughulika na usaliti katika uhusiano wako. Hata kama mumeo au mkeo au umpendaye ni msaliti, unaweza kushughulikia tatizo hilo bila kusababisha madhara makubwa kama ndoa kuvunjika au kuachana kwa ugomvi na kuacha watoto wakiteseka au kuvuruga ndoto zenu nyingi mlizokuwa nazo pamoja.

 

Inapotokea umegundua kwamba mwenzi wako  amekusaliti, hata ukiwa umekasirika kiasi gani, unatakiwa kutuliza akili kwanza na kufanya yafuatayo; Muite mwenzi wako na umweleze kwamba umegundua mambo anayokufanyia nyuma ya pazia, ni dhahiri kwamba atajisikia vibaya sana kwa sababu hakuna anayependa kuonekana msaliti kwenye mapenzi.

 

Hatua ya pili, hakikisha mwenzi wako anakubali kusitisha mawasiliano na huyo mtu wake mara moja! Unatakiwa kusimamia kuhakikisha hawawasiliani tena na hapo ndipo hatua nyingine zinapoweza kufuata. Ukiona umeshampiga marufuku kuendelea kuwasiliana naye, lakini bado anaendelea hapo sasa ndipo unapoweza kuanza kufikiria hatua nyingine kubwa zaidi.

Endapo utajiridhisha kwamba hawawasiliani tena kwa namna yoyote, utakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kushughulikia tatizo hilo kikamilifu. Hii inawahusu pia wasaliti, unapoona mwenzi wako amegundua kwamba unamsaliti, kitu cha kwanza kabisa ni kukata mawasiliano na huo mchepuko! Vinginevyo unaweza kuipoteza kabisa ndoa yako au huo unaweza kuwa mwisho wa uhusiano wenu.

 

Umuhimu wa hatua hii ni kumpa mwenzi wako nafasi ya kuthibitisha kwamba alikusaliti kwa kukusudia au ameteleza tu. Mtu ambaye amekukosea kwa bahati mbaya, ataonesha dhahiri kwamba anajutia makosa yake, atahitaji sana umsamehe na haya atayaonesha kwa vitendo.

 

Ikitokea anashindwa kuonesha kujutia makosa yake, anaendelea kuwa kiburi, wanaendelea kuwasiliana, basi ni dhahiri kwamba huyo hakufai, unatakiwa kukubali tu aende zake na kwenye matoleo yajayo nitakuelekeza namna ya kumtoa na kumsahau mtu wa aina hii kwenye mapenzi.

 

Lakini kama ataonesha kujutia, narudia tena kusisitiza kwamba bado unayo nafasi ya kumsamehe na kufungua ukurasa mpya. Kivipi? Kwanza utahitaji kupata muda wa kutosha wa kukaa peke yako kutafakari kwa kina nini kimesababisha akakusaliti, kwa sababu wakati mwingine inawezekana wewe ndiye chanzo cha yeye kuchepuka ingawa hioyo haihalalishi kosa.

 

Katika hatua za mwanzo unaweza kujikuta ukimchukia sana, lakini hakuna kitu kinachosahaulisha machungu ya moyo kama muda! Jipe muda na taratibu moyo wako utaanza kupona majeraha ya kusalitiwa.

 

Baada ya kujipa muda wa kutosha, unapaswa kumpa nafasi mwenzi wako ya kuelezea tukio lilivyotokea na nini kilichosababisha. Wengi huwa wanakosea kuchukua uamuzi wa haraka, unaposalitiwa unatakiwa kujiepusha na uamuzi wa haraka, jipe muda na hakika hakuna tatizo kubwa kukuzidi wewe.

ITAENDELEA WIKI IJAYO.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.