The House of Favourite Newspapers

ANASWA KWA WIZI FEDHA MTANDAONI

MOROGORO: Kijana mmoja ‘Sharobaro’ ambaye jina lake halikupatikana mara moja amepokea kochapo kutoka kwa wananchi waliomshutumu kuiba pesa kwa njia ya mtandao wa simu. 

 

Tukio hilo lililojaza umati mkubwa wa watu limetokea juzikati Mtaa wa Umbonga eneo la Kikundi Kata ya Sultan Mkoani hapa. Wakihojiwa na Mwandishi wetu, mashuhuda wa tukio hilo walidai kwamba, kwa sasa wimbi la wizi wa pesa kwa njia ya mtandao umeshamiri mkoani hapa, hivyo sharobaro huyo arobaini yake ilifika siku hiyo.

 

“Huyu jamaa ni …(anamtuhumu wizi) maarufu wa pesa kupitia mitandao ya simu anaenda kwa mawakala anafanya anavyojua na kuwaibia pesa.

 

“Leo alifanya hivyo hapa mtaani kwa wakala Abraham Yohana na kufanikiwa kutoa fedha (kiasi hakukitaja kwa usahihi), lakini kwa kuwa wakala huyo alishaibiwa sana kwa staili hiyo alikuwa makini kwa lengo la kumnasa mtuhumiwa huyo. “Jamaa alipotinga kwa wakala huyo akitumia staili ileile waliyotumia wenzake wa nyuma waliomwibia wakala huyo.

“Baada ya kubaini ujanja wa huyo jamaa, Abraham alimkamata na kupiga mayowe ya ‘mwizi’, wananchi wakajitokeza na kuanza kumpa kipigo na kumpeleka kituo cha polisi,” alisema Abubakar Juma, maarufu kwa jina la Iniesta.

 

Aliongeza kwa kusema, wakati wanampeleka mtuhumiwa huyo Kituo Kidogo cha Polisi Kikundi majira ya mchana walikuta kituo hicho kimefungwa hivyo kulazimika kumpeleka mtuhumiwa huyo kituo kikuu cha polisi mkoani hapa. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Salome Thomas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye mtaa wake.

 

Alipoulizwa kuhusiana na kituo cha polisi kilichokarabatiwa hivi karibuni kufungwa mchana, mwenyekiti huyo alijibu: “Umeanza udaku wako, kituo chetu kinafanya kazi, taarifa nilizo nazo ni kwamba askari wa kituo hicho jana na leo hakufungua kwa kuwa anauguliwa.”

 

Gazeti hili lilitinga kwa wakala Abraham kwa lengo la kuzungumza naye kujua mbinu aliyotumia mtuhumiwa huyo kujipatia fedha kwa njia haramu lakini lilimkosa kwa madai kwamba ameitwa polisi kutoa maelezo ya tukio hilo. Lakini uchunguzi ambao umekuwa ukifanywa na waandishi wetu sehemu mbalimbali nchini umebaini kuwa, wezi hao wamekuwa wakitumia mbinu nyingi kujipatia fedha ikiwemo hii:

MAELEZO YAKE

Anapofika kwa wakala anauliza kama analo salio la kutosha. Baadaye anamwambia wakala nitumie fedha kwenye simu yangu, anataja namba. Lakini namba hiyo anayotaja anaikosea makusudi namba moja.

 

Kwa wakala ambaye hayuko makini anatuma hiyo fedha. Baadaye yule mwizi anasikilizia taarifa ya kupokea fedha haifiki. Anaanza kulalamika. Anamwambia wakala; we kwani umetuma kwenye namba gani? Wakala anapoisoma hiyo namba, yule mwizi anamwambia umekosea namba ya mwisho.

 

Wakala anapojaribu kufuatilia muamala wake anakuta yule aliyemtumia ambaye ni mshirika wa yule mwizi anakuwa ameshaitoa na hivyo kujikuta hawezi kulipwa na yule aliyemwambia amtumie kwa sababu fedha hazikuingia kwake, ndiyo anakuwa kaibiwa tena

Comments are closed.