ANASWA WIZI WA MTOTO MCHANGA

AIBU! Mwanamke mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja, Mkazi wa Urambo mkoani Tabora amenaswa kwa wizi wa mtoto mchanga.  Tujiunge na mama Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa majonzi, mama wa mtoto, Salome Sindigu alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita nyumbani kwake Kata ya Miguwa, kitongoji cha Ngong’ho wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.

Akisimulia kisa hicho Salome alikuwa na haya ya kusema: “Hapa nyumbani naishi na watoto wadogo, mmoja ni huyu mchanga. Siku hiyo alikuja mama mmoja akiwa ameshika mfuko na kuniomba msaada wa kumsitiri kwa kuwa huko kijiji alichotoka amepigwa na mumewe.

“Kwa huruma yangu nikamuelewa na kulala naye. Ulipofika usiku akaniambia ametumiwa meseji na jirani yake kwamba mumewe anamtafuta ampige hivyo asubuhi aende kwao mara moja kumchukua mtoto wake.”

AENDA KWA WAKALA

Salome alisema ilipofika asubuhi hakuweza kufikiria mwanamke huyo anachokitaka kwake kwani hakuwa na safari tena ya kurudi kwao bali alimwomba amuelekeze kwa wakala wa simu ili akatoe pesa. “Nilimuelekeza lakini hakurudi hadi ilipofika mchana nikawapikia chakula wanangu nikaenda kwenye harusi. Muda wa kurudi nikashangaa na yeye kumkuta nyumbani akaniambia ameshindwa kutoa pesa kwani hawakuwa na salio hadi kesho yake angeweza kuwekewa.

MTOTO ALIVYOIBIWA

Aliendelea kusimulia kuwa, kesho yake yule mama alibadili tena mawazo ya kuondoka, akamuomba amtafutie chumba cha kupanga, hivyo wakatafuta na kufanikiwa kukipata kimoja. “Tuliporudi nyumbani na kuingia ndani akaniomba ambebe mwanangu, sikuwa na shaka nikampa kisha nikaingia chumbani nikiwa sina wasiwasi naye.

AFUNGIWA MLANGO KWA NJE

“Kitendo cha kurudi sebuleni nikakuta mfuko wake haupo, kushika kitasa cha mlango nikagundua kuwa kanifungia kwa nje ikabidi nianze kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani. Sikufanikiwa kitu hadi nilipobomoa dirisha na kwenda kwa majirani kuomba msaada, ukafanyika msako wa kumtafuta huyo mwanamke.

SOO LATINGA POLISI

“Tulikwenda kituo cha polisi wilayani Nzega kuripoti na tulipofika tukaambiwa tuendelee kumtafuta na ikifika jioni tuwapelekee taarifa kama tumempata au la. “Basi ilipofika kama saa nne usiku tukapigiwa simu kwamba mtuhumiwa amekamatwa tukaenda huko alikokamatiwa na tukamchukua mwanangu.”

MSIKIE MWIZI WA MTOTO

Akizungumza mara baada ya kunaswa na mtoto huyo, mwizi huyo alieleza sababu iliyomfanya kuiba mtoto wa Salome huku akikataa kutaja jina lake. “Natokea Urambo, Tabora hapa nimeletwa na wapita njia tu. Siyo kama nimemuiba bali nilikuwa napenda tu mtoto. Mtoto wangu nilijifungua zamani kwa bahati mbaya akafariki dunia. Hivyo niliamua kumchukua huyu.”

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Miguwa, Tambwe Ramadhan aliwashukuru wananchi kwa kujitoa na kuhakikisha mwanakijiji mwenzao amepata mtoto wake na akasema ili kuondoa tatizo hilo kuwe na vitambulisho vya wakazi.

“Kikubwa kuwe na ushirikiano, ukimuona mtu usiyemjua, toa taarifa serikalini kwanza. Hii itatusaidia sana kwa wakazi wa eneo hili kuwatambua wageni na kuwathibiti,” alisema Tambwe. Diwani wa Kata ya Miguwa, Revocatus Ngai aliwataka wananchi kuwa makini na wageni na kuhakikisha wanajua kilichowapeleka majumbani mwao kwa usalama wao.


Loading...

Toa comment