The House of Favourite Newspapers

Dunia Haina Huruma… Anayepumulia Mashine Afanyiwa Kitu Mbaya

DAR ES SALAAM: DUNIA Haina Huruma! Mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Bahati Bukuku alipata kuimba wimbo huo, ambao unasadifu maumivu na mateso ambayo mtu anaweza kufanyiwa na walimwengu.  Hamadi Hawadhi (28), mkazi wa Ukonga, jijini Dar, anayeishi kwa kutumia mashine ya kupumulia ambaye anasaka msaada kwa wasamaria wema ili aweze kwenda nje ya nchi kutibiwa kufuatia mapafu yake kusinyaa na moyo kuhamia upande wa kulia, ametapeliwa Tsh. 50,000 na watu waliojitokeza na kujifanya wana nia ya kumsaidia.

Hamadi, kwa mara ya kwanza aliripotiwa na gazeti dada la hili, Ijumaa Wikienda toleo la Jumatatu iliyopita, likiwa na kichwa cha habari, ‘WAKICHOMOA MPIRA NAKUFA’, akihitaji msaada kwa wasamaria wema.

AKUMBANA NA MATAPELI

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati akisubiri misaada kutoka kwa watu walioguswa na tatizo lake, alikutana na matapeli hao.

Akizungumza na Amani, nyumbani kwake, Hamadi alisema: “Yaani roho inaniuma sana. Nikiwa katika hali hii ya mateso ya kuishi kwa kuomba msaada ili nikatibiwe wiki iliyopita alinipigia simu mwanamke mmoja aliyejitambulisha kuwa anatoka Ubalozi wa Emirates (Falme za Kiarabu) na kusema kuwa walikuwa na nia ya kunisaidia.”

MILIONI 11 ZATAJWA

“Nikiwa nimetega sikio kuisikilizia neema hiyo, mwanamke huyo aliniambia wanataka kunisaidia kwa kuanza na kunipa milioni 11, kisha baadaye wangeona namna ya kuongeza nyingine nikiwa tayari hospitalini,” alisema Hamadi huku akiugulia na kushika sehemu za mbavu akisema zinambana.

 

Hamadi anaendelea kusimulia: “Aliniuliza kama nina akaunti, nikamjibu na kumtajia jina la akaunti na benki iliyopo, akasema wao hawafanyi kazi na benki hiyo, akaniagiza nifungue akaunti ya benki ya (tunaificha kwa sasa kwa sababu maalum).”

 

Bila kuelewa nia ovu aliyokuwa nayo mwanamke huyo, Hamadi alikubaliana na sharti la kufungua akaunti katika benki aliyomwelekeza. “Nilimwambia nipo Ukonga, yeye akanielekeza tawi la karibu na hapa nikafungue akaunti. Aliniambia nikifika pale benki, nitakutana na meneja wa tawi hilo, ambaye angenisaidia kufungua hiyo akaunti.

 

“Kweli nilipofika hapo benki, nikakutana na huyo meneja ambaye yeye alisema anamfahamu. Hiyo ni baada ya kumpigia simu, maana alinitumia namba zake. “Huyo meneja baada ya kujitambulisha, alisema akaunti hiyo inaweza kufunguliwa haraka kwa gharama ya Tsh. 50,000 na kututaka twende ofisini kwake lakini kwa kuwa mimi siwezi kutoka kwenye gesi niliwaagiza mke wangu na mjomba wangu ambao ndiyo wanaoniuguza hapa nyumbani,” alisema Hamadi.

 

Baada ya kuingia ndani ya benki hiyo, anaeleza kuwa meneja huyo aliwaambia hakuna haja ya kuingia ofisini kwake kwa kuwa alikuwa na kazi nyingi, hivyo aliwapa namba ya simu ili wamtumie hiyo fedha na yeye awafungulie akaunti hiyo haraka.

UTAPELI WABAINIKA

“Lakini baada ya kumtumia hiyo fedha, mke wangu na mjomba wangu walikaa sana kumsubiri hakutokea. Hawakuelewa alipoelekea, lakini muda ulivyozidi kusonga wakaamua kumpigia, hakupatikana.

 

“Wakaja nje nilipokuwa, tukajaribu kumpigia tena, hakupatikana. Hata namba ya yule mama Mwarabu nayo pia tuliipiga sana, haikupatikana,” alisema kwa masikitiko makubwa Hamadi. Anasema, hata walipoingia ndani ya benki hiyo na kutoa maelezo hayo, walielezwa hawana meneja wa namna hiyo.

 

MSAIDIE HAMADI

Hamadi bado anahitaji msaada wako Mtanzania. Kama umeguswa, unaweza kuwasiliana naye au kumtumia mchango wako kupitia namba 0712827841 – jina lililosajiliwa ni CATHERINE KULEKANA.

Comments are closed.