ANG’ATWA MKONO NA MWANAMKE, WANYAUKA

MWANAUME mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Saliini Athuman, mkazi wa Mbagala jijini Dar, amepata kilema cha mkono baada ya kung’atwa na mwanamke aliyetajwa kwa jina la Zai. Tukio la Saliini kung’atwa mkono wake huo hadi kunyofolewa nyama lilitokea mwishoni mwa mwaka jana huko Emauta mkoani Mtwara kisa kikidaiwa ni kugombea simu.

 

MKASA ULIVYOKUWA

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Saliini alisema: “Yaani mimi huyo mwanamke nilikuwa niko naye, sasa kuna wakati nilimnunulia simu mpya lakini akawa haitumii, badala yake akawa anatumia simu nyingine na wakati huo kuna watu walikuwa wakidai kuwa ananisaliti.

 

“Sasa siku moja nilipotaka kuichukua ile simu anayotumia akawa mkali sana, nilipolazimisha ndipo akaning’ata mkononi. “Mara ya kwanza alining’ata akatema lile pande la nyama, mara ya pili aling’an’gania mkono kwa dakika kama 45 hivi bila kuachia, hata watu walipokuwa wakiamulia ilishindikana, baadaye ndiyo akaniachia na kukimbia,” alisema baba huyo

 

kwa uchungu. Akaongeza kuwa, baada ya mwanamke huyo kufanya kitendo hicho cha kinyama alimuacha akiugulia kwa maumivu makali na baadaye mkono ulivimba. “Yaani mkono ulivimba na ndani ya muda mfupi ulikuwa kama paja la mtoto mdogo, wakati huo damu ilikuwa ikitoka nyingi sana kwa sababu iliathiri mfupa mkubwa.

 

“Nilipoenda hospitali baada ya madaktari kuona hali mbaya niliyokuwa nayo kwanza nilichomwa sindano mbili za tetenasi. Baadaye wakaniambia niende hospitali ya Newala lakini pale ilishindikana kupata matibabu sahihi, ikabidi niende Tandahimba ambako walinipiga X-Ray na kugundua kuwa mshipa mkubwa ambao unaenda kwenye moyo ulikuwa umekatika.

 

“Majibu hayo yaliwalazimu kunifanyia upasuaji mdogo lakini bado vidole vyote vikawa havifanyi kazi. Kutokana na hali hiyo niliamua kuja Dar na kuanzia hospitali ya Temeke kisha baadaye nikahamishiwa Muhimbili.

 

“Pale Muhimbili nilitakiwa nitengenezewe kitu cha kusapoti mkono wangu ambacho ni gharama lakini pia nikatakiwa kutumia dawa flani ambazo kwa bei ya harakaharaka ilifikia shilingi 245,000, pesa hiyo imekuwa ngumu kwangu, nimebaki nataabika tu,” anasema baba huyo.

 

Anasema kuwa, uwezo wa yeye kupata pesa hizo ni mdogo na ndiyo maana amekuwa akiomba Watanzania ambao wameguswa na tatizo lake wamsaidie. Alipoulizwa hatua ambazo zilichukuliwa baada ya mwanamke huyo kumfanyia ukatili huo, Saliini alisema:

 

“Baada ya tukio hilo, kesi ilienda mahakamani, ikanguruma lakini mwisho wa siku hukumu ilitolewa kwamba yule mwanamke aende kifungo cha nje cha miezi sita na pia alipe faini ya shilingi elfu hamsini.

 

“Hiyo pesa yenyewe sijawahi kulipwa, nipo tu nateseka na maisha yangu.” Kwa mtu yoyote aliyeguswa na tatizo la baba huyu anaweza kumpata kupitia simu yake ya mkononi kwa namba 0655369034. Kumbuka kwamba, kutoa ni moyo wala siyo utajiri.


Loading...

Toa comment