The House of Favourite Newspapers

Anna Maboya…Muimba Injili Bongo Mwenye Malengo Ya Kimataifa

Mwimbaji wa Nyimbo za Injili, Anna Maboya

ANNA Maboya ni mwimbaji wa Nyimbo za Injili ambaye malengo yake makubwa ni kuona anaufikia ulimwengu kwa wakati akipaza sauti na kuimba bila kuchoka jambo ambalo limekuwa ni furaha yake muda wote.

 

Kwa sasa ameongozwa na roho mtakatifu kwenye utunzi wa nyimbo mbili ambazo ni Sifa na Hakuna Usiloliweza. Nyimbo zote hizo zimepokewa vizuri na mashabiki jambo linalompa furaha ya kufikiria kazi kubwa ya kutunga albamu itakayowaokoa wengi.

 

Championi Ijumaa, limefanya mahojiano maalumu na mwimbaji huyo ambaye kipaji chake kilianza tangu akiwa mdogo mpaka leo anatimiza ndoto ya kile alichokuwa anakifikiria. Huyu hapa anafunguka:

Mhariri wa Championi Ijumaa John Joseph (kushoto) akiwa na Mtangazaji wa Global TV Online, Given Masishanga  wakiwa katika picha ya pamoja na Anna Maboya.

“Kazi kubwa ambayo inanipa furaha muda wote kuifanya ni kuimba na nimekuwa nikifanya hivyo tangu nikiwa mdogo na mpaka sasa nimekuwa naendelea kufanya huduma ya kuimba, ni kitu kinachonipa furaha.

 

“Nilianza kuimba katika Sunday School, nikaendelea mpaka nilipomaliza elimu ya msingi katika Shule ya Sua mkoani Morogoro na baadaye Shule ya Sekondari TASI iliyopo Arusha.

Meneja wa Global Publishers, Abdallah Mrisho (kushoto) akiongea jambo na Anna Maboya.

Ilikuwaje ulipofika sekondari?

“Pale tulikuwa na kundi letu ambalo lilikuwa na waimbaji sita na muunganiko huo ulitambulika kwa jina la Celestial School.

 

Kwa sasa kundi hilo lipo wapi?

“Baada ya kumaliza kidato cha nne, hilo kundi nalo likawa limeishia hapo kwani hatukuweza kukaa pamoja, kila mmoja aliendelea na shughuli zake, wapo ambao walikwenda kusoma nje ya nchi na wengine tukatengana mikoa mbalimbali, hivyo ikawa ngumu kuwa karibu tena.

 

Baada ya hapo ikawaje?

“Nilipokuwa kidato cha tano na sita, tuliunda kundi lingine na safari hii nilikuwa na waimbaji wenzangu ambao ni Lily Max na Asibisye. Tuliendelea kufanya kazi, lakini hatukutoa albamu zaidi ya kuimba tukiwa ni kundi moja.

 

Kwa nini unapenda kuimba nyimbo za kuabudu na kusifu?

“Asili ya Mungu wetu ni Mungu wa Sifa na kuabudiwa, hivyo imekuwa ni karama yangu kuimba na kusifu, pia hata nikiwa kanisani nimekuwa kiongozi wa kundi la kusifu na kuabudu ndiyo maana ninaimba nyimbo hizo.

 

Nani anakuandikia nyimbo zako?

“Nyimbo zote mbili mimi ndiye mtunzi, ukianza na ule wa kwanza wa Sifa, hata huu wa sasa ambao bado mpya unaoitwa Hakuna Usiloliweza.

 

“Huu wa sasa ambao ni mpya, niliuandika usiku wa manane baada ya kushtuka kutoka usingizini.

 

Kwa nini Hakuna Usiloliweza?

“Ni ukweli ambao upo kwenye maisha ambayo tunayaishi siku zote, wengi wanapitia kwenye magumu, hata mimi pia nina magumu ambayo nilipitia ila mwisho wa siku Mungu akatenda miujiza na kwa neema yake nipo hapa nilipo, hivyo ni kwa kila mmoja ndio maana nikaupa jina hilo.

 

Unafanya uimbaji wa aina gani?

“Mimi uimbaji wangu ni maalumu kwa ajili ya kumtukuza bwana, sina mpango wa kufanya uimbaji wa biashara, hivyo ninachopenda ni mapokezi ya mashabiki pamoja na jamii kuelewa kazi zangu ambazo ninazifanya.

 

Nani anakugharamia kazi zako?

“Najigharamia mwenyewe, pia wazazi wangu ambapo baba, yeye ni Askofu wa Kanisa la CAG (Calvary Assemblies of God) na mama Imelda Maboya ni Mchungaji wa Kanisa la CAG Tawi la Ubungo Maziwa, wamekuwa wakinisapoti japokuwa nimekuwa sipendi kuwasumbua sana.

 

Je, una familia kwa sasa?

“Bado wakati wa Bwana haujafika, Mungu akiamua nitakuwa na familia yangu wakati ujao.

 

Malengo yako ni yapi?

“Ni kutoa albamu bora ambayo itakuwa ni ya kipekee Afrika kutokana na utunzi na kazi ambazo ninazifanya.

 

“Mpango wangu ni kushirikiana na waimbaji wengine kwenye kazi zangu ila albamu yangu ya kwanza nitafanya peke yangu kisha zinazofuata nitawashirikisha wengine na miongoni mwa ninaopenda kufanya nao kazi ni Angel Bernard, Lily Max na Sinach.

 

Unawaambia nini mashabiki wako?

“Wanipe sapoti katika kazi ambazo ninafanya kwani kwenye albamu yangu nitakuwa na nyimbo tisa na zitakuwa kwenye mafungu matatu, fungu la kwanza ni za kuabudu, la pili ni kusifu na la tatu ni zile za kuchangamka,” anamaliza Anna.

Comments are closed.