The House of Favourite Newspapers

Anne Makinda Afurahia Ubora Wa Wahitimu HKMU

0
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Anne Makinda akimtunuku Shahada ya udaktari bingwa mmoja wa wahitimu wa udaktari bingwa kwenye mahafali ya 20 ya chuo hicho.

 

CHUO Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), kimeiomba serikali kuendelea kuongeza mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wa fani za afya hali ambayo itapunguza uhaba wa watumishi kwenye sekta hiyo nchini.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, John Ulanga, kwenye mahafali ya 20 ya chuo hicho ambapo wahitimu 294 walitunukiwa shahada mbalimbali.

Sehemu ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU)wakila kiapo kwenye mahafali hayo yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam

 

Katika mahafali hayo, wahitimu 180 walitunukiwa Shahada ya udaktari wa binadamu, 38 Shahada ya Uuguzi, 54 Shahada ya Uuguzi, 10 Stashahada ya Ustawi wa Jamii, 10 Shahada ya Uzamili ya Udaktari wa Binadamu katika Tba na Afya ya Watoto.

Pia kwenye mahafali hayo mwanaume mmoja alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya Upasuaji na mwanamke moja alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Afya ya Jamii

Alisema HKMU imetoa mchango mkubwa sana tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa wataalamu wa afya wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wanaofanyakazi kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mwenyekiti wa Baraza la chuo cha HKMU John Ulanga akizungumza kwenye mahafali ambayo yamefanyika leo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

 

Ulanga alisema wahitimu wa chuo hicho walionyesha umahiri mkubwa sana kwenye kusanyiko la wanataaluma kwa namna ambavyo walimudu kuwasilisha mada zao kwa utaalamu wa hali ya juu hivyo kuonyesha kuwa wamepikwa vya kutosha.

“Juzi wakati ninasikiliza ubora na umahiri wa mawasilisho yao nilijiuliza hivi seriali haiwezi ruzuku kwenye vyuo kama HKMU kutuwezesha kuongeza idadi ya wataalamu tunaozalishana pia kuongeza idadi ya tafiti zinazofanyika, tunaomba Mkuu wa chuo utupigie debe tupate ruzuku serikalini kuendesha chuo,” alisema Ulanga

Aliishukuru serikali kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa chuo hicho na wa vyuo vingine kwani mikopo hiyo inawawezesha wanafunzi kutoka kaya maskini kupata elimu na kuondokana  na maisha duni.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Taaluma, Profesa Ntabaye akibadilishana mawazo na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Yohana Mashalla

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu ya Afya, (KHEN), Kokushubira Kairuki, alisema sababu kubwa iliyoisukuma Kampuni ya KHEN kuwekeza kwenye elimu ya juu hasa afya kuanzia mwaka 1992 ilitokana na uhaba wa watumishi kwenye sekta hiyo nchini.

 

“Katika mahafali yetu ya kwanza mwaka 2003 wahitimu walikuwa 63 wakiwemo madaktari wanne na wengine wakiwa wauguzi lakini leo hii katika mahafali haya ya 20 tuna wahitimu 294 na idadi hii inafkisha jumla ya wahitimu 3,186 miongoni mwao wakiwemo madaktari wa binadamu 1,560,” alisema

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), linapendekeza uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 8,000 na kwamba uwiano huo kwa hapa Tanzania bado hauridhishi kwani daktari mmoja anakadiriwa kuhudumia wagonjwa 20,000 kwa mwaka.

“Ingawa mahitaji bado ni makubwa tunamshukuru Mungu kwamba tumeweza kuendelea kutoa mchango wetu kwa taifa katika kupunguza uhaba wa rasilimali watu katika sekta ya afya mwaka hadi mwaka kwa miaka 25 mfululizo,” alisema

Mkuu wa chuo hicho, Anne Makinda alisema chuo hicho tangu kuanzishwa kwake kimekuwa kikitoa wahitimu bora wenye weledi wa hali ya juu ambao wanafanyakazi kwenye maeneo mbalimbali ndani na n je ya nchi.

 

“Juzi tulikuwa na kusanyiko la kitaaluma walikuja waliowahi kusoma HKMU kwa kweli ukiwasiliza wanavyowasilisha mada zao wanavyojiamini unapata uhakika kabisa kwamba hapa ni sehemu sahihi ya kufundisha watumishi wa kada ya afya,” alisema

 

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Yohana Mashalla, aliomba serikali ipunguze gharama za vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili wanafunzi wengi zaidi waweze kusoma kwa njia ya mtandao.

Profesa Mashalla aliiomba serikali kuvipa ruzuku kwa vyuo viuu binafsi ili vijiandae kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu, kusomesha wahadhiri na ununuzi wa vifaa vya kufundishia, maabara na maktaba ili kukidhi mahitaji ya kuongezeka kwa mahitaji ya elimu ya  juu nchini.

Aidha, alisema katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wahadhiri, HKMU imeendelea kufadhili masomo ya wahadhiri katika ngazi ya uzamili na uzamivu ndani na nje ya nchi.

Alisema kwa sasa jumla ya wahadhiri 14 wako masomoni, kati yao saba masomo ya uzamivu na wengine saba masomo kwa ngazi ya uzamili.

 

Leave A Reply