The House of Favourite Newspapers

AROBAINI YA MWANAYE…YAMPONZA MBOSSO!

NI shida! Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya hivi karibuni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Yusuf Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ kumfanyia sherehe ya kumtoa nje mwanaye aliyetimiza siku arobaini tangu azaliwe ambayo imemponza; Risasi Jumamosi linakupa habari kamili.

Ilikuwa hivi; sherehe ya kumtoa mtoto wa Mbosso aliyezaa na mpenzi wake, Rukia Rucky ilifanyika nyumbani kwa mwanamama huyo Sinza-Lion, Dar ambapo dua ilifanyika asubuhi kisha jioni ikafanyika ‘laana’ ya kufa mtu mtaani hapo.

MAUNO YA ‘LAANA’

Baada ya kufanya dua asubuhi na sherehe mchana, jioni ilifanyika sherehe nyingine ya laana kwani wanawake kibao waliohudhuria akiwemo msanii wa filamu nchini, Skyner Ally ‘Skaina’ na mwanamuziki Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ walikata mauno ya kufa mtu huku wengine wakiacha maungo yao nyeti njenje.

Licha ya sherehe hiyo kuwa kama ya wanawake tu, wanaume ‘tata’ nao walitawala huku wakikata mauno ileile.

YAMPONZA MBOSSO

Kutokana na ‘laana’ hiyo baadhi ya waalikwa walionekana wakimlaumu Mbosso kuwa ni kwa nini aliamua kuruhusu mwanaye afanyiwe sherehe ya aina hiyo kwani hata kidini hairuhusiwi.

“Jamani huyu mtoto wanampa laana maana haitakiwi afanyiwe sherehe ya hivi, yaani asubuhi amefanyiwa dua halafu jioni anakuja kukatiwa mauno kama hivi…hata hiyo dua haina maana tena kwa kweli,” alisikika mmoja wa waalikwa aliyekuwa akiwakodolea wenzake macho wakiwa wanakata mauno kihasara.

Katika mitandao ya kijamii hasa Instagram nako palichafuka baada ya video ya wanawake hao wakikata mauno kihasara kusambaa na watu kusema Mbosso hakutakiwa kumfanyia mwanaye sherehe ya aina hiyo.

MBOSSO ALIKUWA HATAKI

Chanzo cha ndani kilieleza kuwa Mbosso hakutaka shughuli hiyo ya jioni ifanyike na ndiyo maana hakutokea na alimzuia mzazi mwenzake lakini hakusikia kwa kuwa walikuwa wameshajiandaa na marafiki zake.

“Mbosso alimkataza mzazi mwenzake asifanye sherehe hii ya usiku na ndiyo maana haikufanyika pale ilipokuwa dua mchana imekuja kufanyika huku kwa jirani maana amelazimisha, yaani hii ni shida maana dua ya mtoto haitakiwi kuwa hivi,” alisema mtoa habari wetu.

MBOSSO ASAKWA

Risasi Jumamosi lilimsaka Mbosso ili kuzungumzia ‘laana’ hiyo ambapo alipokea simu na kueleza kuwa yupo safarini atazungumza baadaye lakini mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni hakufanikiwa kuzungumza.

STORI: Mwandishi wetu, Risasi Jumamosi

Comments are closed.