The House of Favourite Newspapers

Arsenal, PSG, Bayern Zatakiwa Kusitisha Visit Rwanda

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imezitaka klabu za Arsenal, Bayern Munich na Paris St-Germain kusitisha mikataba yao ya udhamini na ‘Visit Rwanda’ kwa kile ilichokiita kuwa ni udhamini uliochafuliwa na damu kwa madai kuwa Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.

Wito huo umetolewa wakati ambapo waasi wa M23 wameuteka mji wa Goma, jiji kubwa zaidi mashariki mwa DRC, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) likikadiria kuwa zaidi ya watu 400,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao mwaka huu pekee.

Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Thérèse Kayikwamba Wagner, ameandika barua kwa wamiliki wa Arsenal, PSG na kwa rais wa Bayern Munich, Herbert Hainer, akitaka maelezo juu ya uadilifu wa mikataba hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Thérèse Kayikwamba Wagner

Katika barua hiyo, Wagner ameonesha wasiwasi kuwa udhamini wa ‘Visit Rwanda’ huenda unafadhiliwa na madini yanayochimbwa kwa njia haramu katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi wa M23, kabla ya kusafirishwa nje kupitia Rwanda.

Kwa Arsenal, Waziri Wagner ameandika: “Ushiriki wa Rwanda katika mzozo huu sasa umethibitishwa bila shaka baada ya ripoti za Umoja wa Mataifa kudai kuwa wanajeshi 4,000 wa Rwanda wako DRC.

“Ni wakati sasa kwa Arsenal kusitisha udhamini huu uliochafuliwa na damu. Ikiwa si kwa dhamira zenu binafsi, basi klabu inapaswa kufanya hivyo kwa heshima ya waathiriwa wa ukatili wa Rwanda,” aliandika Wagner.