Arsenal Yapewa Kigongo Europa

ARSENAL ambayo usiku wa kuamkia jana Ijumaa iliifunga Rennes mabao 3-0 na kuiondosha timu hiyo kwa jumla ya mabao 4-3 kwenye michuano ya Europa hatua ya 16 Bora, imepangwa kucheza na Napoli hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

 

Katika droo ya michuano hiyo iliyopangwa jana, inaonyesha kuwa, Arsenal itaanzia ugenini, kisha zitarudiana kule London na mshindi wa jumla atafuzu nusu fainali.

 

Wakati Arsenal ikiangukia kwa Napoli, Chelsea nayo imepangwa kucheza na Slavia Praha ya Jamhuri ya Czech.

 

Chelsea itaanzia ugenini. Mechi zingine za hatua hiyo ni Benfica dhidi ya Frankfurt, huku Villarreal ikicheza na Valencia. Katika michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi ni Atlético Madrid, mechi za kwanza za hatua hiyo zimepangwa kuchezwa Aprili 11 na marudiano ni Aprili 18, mwaka huu.

 

Katika nusu fainali, mshindi kati ya Arsenal na Napoli atapambana na Villarreal au Valencia, huku mshindi baina ya Chelsea na Slavia Praha, atakutana na Benfica au Frankfurt.

Fainali ya michuano hiyo itafanyika Mei 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Olympic uliopo katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Toa comment