The House of Favourite Newspapers

Arteta: tulistahili kupewa penalti

0

Kocha wa klabu ya Arsenal, Mikel Arteta (42) amesikitishwa na kuonesha kutoridhishwa na maamuzi yaliyofanywa na waamuzi waliosimamia mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa hapo jana dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia, Internazionale Milan katika mchezo waliopoteza kwa goli 1-0 ugenini.

Kocha alionesha hali ya kutokufurahishwa haswa na penalti waliyopewa Inter Milan mwishoni kwa kipindi cha kwanza iliyozaa bao pekee katika mchezo huo huku pia akieleza kwamba tukio la kiungo wa timu yake, Mikel Merino kupigwa ngumi na golikipa wa Inter, Yann Sommer lilipaswa kuamuliwa kama penalti na mwamuzi wa kati kutoka Romania Istvan Kovacs aliyesimamia mchezo huo.

“Nimechanganyikiwa sana kwa sababu kuna maamuzi mawili ambayo yaliamua mwenendo mzima wa mchezo. Sielewi, hakukuwa na hatari hata kidogo. Hauwezi kujibu kwa sababu mpira uko karibu sana. Lakini sawa. Waliamua hiyo ni adhabu ya penalti. Lakini ikiwa hiyo ni penalti basi ile ya Mikel Merino ambapo alipigwa (na Yann Sommer) kichwani ilibidi iwe penalti kwa asilimia 100. Huo ndo utofauti katika mchezo huu na ni vigumu sana kukubali.” Alisema kocha huyo akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo.

Aidha, Arteta pia amewapongeza wachezaji wake kwa kiwango kizuri walichokionesha dhidi ya klabu kubwa barani Ulaya katika uwanja wa ugenini baada ya vijana wake kuonekana kutawala mchezo wakipiga mashuti 20, umiliki wa mpira asilimia 63 dhidi ya 37 za wapinzani wao, kona 13 dhidi ya 0 kwa wapinzani wao waliofanikiwa kupiga shuti moja tu lilolenga lango katika mchezo huo.

Leave A Reply