The House of Favourite Newspapers

ASHA BARAKA: TWANGA WAMENITENDEA HAKI

Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka akimlisha keki, mwanamuziki wa bendi yake, Haji Makuke.

Jana usiku ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, Asha Baraka ambapo kwenye Ukumbi wa The Legends Club uliopo Namanga jijini Dar, Twanga hupiga shoo kila Jumapili, alikata keki pamoja na familia yake na wanamuziki wa bendi hiyo. Akizungumza baada ya kukata keki aliyoandaliwa na wanamuziki wake pamoja na familia yake, Asha Baraka alisema kwamba anawashukuru wanamuziki wake kwa upendo waliomuonyesha pamoja na familia yake pia.

“Kiukweli ni upendo wa ajabu nimeonyeshwa na wanamuziki wangu ambao kwangu mimi ni sehemu ya familia yangu ya damu. Ninawapenda na nitaendelea kushirikiana nao kwa kila hatua mpaka tufikie malengo yetu. “Lakini pia kwa familia yangu, ndugu na jamaa na wapenzi wote wa Twanga Pepeta ninawashukuru kwa upendo walionionyesha kwenye siku yangu hii ya kuzaliwa,” alisema Asha Baraka.

Asha Baraka akimlisha keki, Angel Bushoke

Kwa upande wa mwanamuziki mkongwe wa Dansi, Komandoo Hamza Kalala, baba wa mwanamuziki wa Twanga, Kalala Junior aliyekuwepo ukumbini hapo, alimtakia Asha Baraka umri mrefu zaidi pia alimpongeza kwa kusimama kidete mpaka Twanga Pepeta inazidi kuimarika siku hadi siku. “Nampongeza mdogo wangu Asha kwa kuongeza umri, hii ni siku yake muhimu sana. Lakini pia pongezi nyingi ziende kwake kwa kuzidi kusimama na kuikingia kifua Bendi ya Twanga Pepeta na inazidi kuimarika siku hadi siku.

“Kumiliki bendi si jambo la mchezo, Mungu akuongoze mdogo wangu siku zote uendelee kuwapa wapenzi wa dansi burudani,” alisema Hamza Kalala. Hata hivyo, Twanga  inatarajia kufanya tamasha la kihistoria la kuadhimisha miaka ishirini tangu kuanzishwa kwake kwenye ukumbi wa The Life Club, Mwenge, Agosti 6, mwaka huu, litakalorushwa ‘live’ na Wasafi TV.

Matukio katika picha:

Asha Baraka akiendelea kulisha keki, ndugu, jamaa na wadau wa wake.
Mwanamuziki wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu akionyesha tisheti za miaka 20 ya Bendi hizo.
Komandoo Hamza Kalala, akicharaza gitaa kwenye shoo ya Twanga alipopanda kujumuika na bendi hiyo.
Mwanamuziki wa Twanga, Kalala Junior akikung’uta Piano.

Stori: Boniphace Ngumije

 

 

Comments are closed.