The House of Favourite Newspapers

ASINGIZIWA KUMBAKA BINTIYE, AFUNGWA MAISHA, MKE AKOMBA MALI

DUNIA haina huruma! Hivyo ndivyo unavyoweza kuzungumzia mkasa uliomtokea Julius Wambua. Mwanaume huyu anatumikia kifungo cha maisha katika Gereza lenye Ulinzi Mkali la Kamiti nchini Kenya. 

 

Kilichompeleka gerezani, ni baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwanaye wa kumzaa, Dorcas. Mpaka (pichani kulia) sasa ameshatum   ikia miaka 10 lakini kuna siri kubwa iliyojificha nyuma ya pazia.

 

Japokuwa kila mtu aliona kama adhabu aliyopewa Wambua alikuwa anastahili kutokana na unyama alioufanya, wa ‘kumbaka’ mwanaye wa kumzaa, mwenyewe aliendelea kushikilia msimamo wake kwamba hajafanya tukio hilo na kamwe hawezi kufanya unyama kama huo.

 

Kilichomtia matatani zaidi, ni ushahidi wa daktari kuthibitisha kwamba ni kweli mtoto huyo alibakwa, kisha mtoto mwenyewe kukiri kwamba ni kweli baba yake alimbaka! Mahakamani ushahidi wa mtoto na ushahidi wa daktari huwa unapewa uzito sana, Wambua akahukumiwa kifungo cha maisha jela.

 

Miaka 10 baadaye, tukio lisilo la kawaida linatokea. Akiwa anaendelea kutumikia adhabu yake, anapata taarifa kwamba mwanaye Dorcas amekuja kumtembelea gerezani! Ni mtoto yuleyule aliyetoa ushahidi mahakamani kwamba amembaka.

 

Moyo wake unakuwa mzito, lakini kwa kuwa ni damu yake, anaamua kwenda kumsikiliza. “Baba nisamehe kwa kutoa ushahidi wa uongo mahakamani, ni mama ndiye aliyenifundisha niseme umenibaka ili ufungwe!” hicho ndicho anachokisema binti huyo huku akimwaga machozi! Inahuzunisha sana.

Unaweza kudhani kwamba ni stori ya kubuni lakini hili ni tukio la kweli kabisa lililomtokea Wambua! Tuhuma za kumbaka mwanaye zilizofanya akahukumiwa kifungo cha maisha jela, hazikuwa na ukweli wowote, zilitengenezwa na aliyekuwa mkewe kwa kumtumia mwanaye wa kumzaa, Dorcas.

 

Lengo lake kubwa lilikuwa ni mwanaume huyo kufungwa ili yeye apate uhuru wa kuuza mali alizoziacha pamoja na kuishi na mwanaume mwingine ambaye anatajwa kuwa ndiye aliyemrubuni mwanamke huyo mpaka akafikia kumfanyia mumewe ukatili mkubwa kiasi hicho.

 

Mwenyewe anaeleza kwamba matatizo yalianza mwaka 2007 ambapo mkewe alibadilika sana kitabia, vurugu zikawa nyingi ndani ya ndoa mpaka mwisho ikabidi ampe talaka. Wambua anasema kwamba baada ya kuachana, mtalaka wake huyo akawa anamsumbua sana kuhusu mgawanyo wa mali walizochuma pamoja, akitaka wagawane nusu kwa nusu.

Akizungumza na mwandishi wa Kituo cha Runinga cha Citizen TV, Wambua anasema kwamba hakuona sababu ya kusumbuana na mwanamke huyo ambaye walikuwa wamezaa watoto kadhaa pamoja, kwa hiyo aliamua kuuza shamba walilokuwa wakilimiliki pamoja.

 

“Niliuza kwa shilingi za Kenya 150,000 (takribani shilingi milioni tatu na nusu za Kibongo), nikaigawanya fedha hiyo nusu, nikampa shilingi za Kenya 75,000 na mimi nikabakiwa na kiasi kama hicho.

 

“Niliongezea fedha nyingine, nikanunua shamba lingine lenye ukubwa wa ekari moja na kuanza kujenga nyumba kisha ndipo nikaoa mke mwingine. Anaeleza kwamba, mwanamke huyo alitumia fedha zote alizopewa na zilipoisha, alirudi kwa Wambua na kumbwagia watoto kwani kwa kipindi chote hicho alikuwa anaishi nao, akasema yeye hana uwezo wa kuwalea peke yake bila msaada wa mumewe.

“Nilikaa chini na mke wangu mpya na kujadiliana naye, tukakubaliana kwamba tuwachukue watoto na kuishi nao, hilo likafanyika na maisha yakaendelea. Mwaka mmoja baadaye, niliwanunulia wanangu kiwanja chao na nikaanza kuwajengea nyumba ili hata nikifa, wasipate shida kwa sababu nilijua japo mke wangu anawapenda, bado yeye ni mama yao wa kambo,” anasema.

Wambua anaendelea kueleza kwamba, aliwarudisha wanaye shule kwa sababu wakiwa kwa mama yao, hawakuwa wakiendelea na masomo, akawa anaendelea na ujenzi wa nyumba ya watoto wake huku pia akiendelea na ujenzi kwenye kiwanja chake alichokuwa akiishi na mkewe mpya.

 

“Siku moja, mtalaka wangu alikuja na kuwaomba watoto wakamtembelee. Kwa kuwa ilikuwa ni likizo, niliwaruhusu na kumweleza kwamba hawatakiwi kukaa zaidi ya siku mbili kwa sababu nilikuwa nimeshawalipia twisheni, akakubali.”

Wambua anaendelea kueleza kwamba hilo lilipita na wanaye wakarudi, siku moja akiwa ameenda sokoni kumsaidia mkewe kununua mahitaji ya nyumbani, alishtukia akisimamishwa na askari kadhaa, waliomuuliza jina lake kisha wakamueleza kwamba anahitajika kituoni.

 

Wakamkamata na kuondoka naye mpaka kituoni, ambapo baadaya kufika, ndipo alipoelezwa habari za kushangaza kwamba alikuwa amekamatwa kwa kosa la kumbaka mwanaye wa kumzaa, Dorcas. Kesi ikaanza kunguruma ambapo Dorcas alitoa ushahidi mahakamani kwamba ni kweli baba yake amembaka, ukaunganishwa na ushahidi mwingine wa cheti cha daktari ambacho baadaye Dorcas anaeleza kwamba ulikuwa ni wa kufoji.

 

“Walinipeleka kwa daktari, akaniandikia kwamba ni kweli nimebakwa, wakaniambia nini cha kusema mahakamani na kunitishia kwamba nikienda tofauti, mimi ndiyo itabidi nifungwe. Ikabidi nitoe ushahidi wa uongo, moyo wangu unajuta sana!” anasema Dorcas.

Wambui anasema aliiomba mahakama akapimwe DNA ili kubaini kama ni kweli alimuingilia mwanaye lakini jaji aliyekuwa anasikiliza kesi yake, alikataa, kwanza kwa kueleza kwamba ni gharama sana lakini hata Wambui aliposema atalipa yeye gharama, aliambiwa kwamba muda wa kupima DNA ulishapita!

 

Akakutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela! Huku nyuma, baada ya kuhukumiwa, mtalaka wake alianza kuuza mali zote alizoziacha, ikiwemo nyumba aliyowajengea wanaye, akamfanyia fujo sana mke wa pili wa Wambua ambaye baadaye alilazimika kuondoka kwenye nyumba yao, nayo ikauzwa.

 

“Nimekuja kukiri kwako baba na kuomba msamaha kwa sababu tunateseka sana. Nimepitia mambo mengi sana ukiwa gerezani, mama alishaolewa na mwanaume mwingine, ndugu zangu wote kila mmoja aliondoka kivyake, nikabaki peke yangu nateseka! Nisamehe baba,” alisema Dorcas huku akilia.

Wambua anasema, hakuwahi kudhani kwamba binti yake anaweza kutoa ushahidi kama huo na anakumbuka kwamba hata wakati akitoa ushahidi mahakamani, muda wote alikuwa amejiinamia chini na hakutaka kutazamana naye, jambo lililomfanya agundue kwamba kuna mchezo umefanyika na mwanaye alikuwa ameshinikizwa.

 

Anasema aliamini kwamba akipimwa DNA itafahamika ukweli kama ni kweli yeye ndiye aliyembaka lakini jaji akakataa, jambo lililofanya ahukumiwe. “Dorcas ni mwananngu, nilimkubali tangu siku ya kwanza anazaliwa, nisingeweza kumfanyia jambo lolote baya na hata leo anaporudi kwangu, nampokea kwa moyo mweupe kabisa.

 

“Hana makosa, alitishwa na kushinikizwa, ila Mungu atanilipia. Nimeishi maisha magumu sana gerezani, ndugu zangu wote wamenitenga wakiamini ni kweli nilimbaka mwanangu, hakuna aliyewahi kunitembelea,” alisema Wambua. Baada ya ushuhuda huo wa mwanaye, amekata rufaa dhidi ya hukumu yake na matarajio yake makubwa ni kwamba siku chache zijazo, atarudi uraiani akiwa mtu huru na kuanza upya kuyajenga maisha yake yaliyopoteza kabisa dira!

Comments are closed.