The House of Favourite Newspapers

Askofu Ataka Rais Magufuli Kuungwa Mkono

0
Rais John Magufuli.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Agustino Shao amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua za kurekebisha mambo muhimu kwa maendeleo ya Taifa, licha ya kuwepo changamoto katika kipindi cha mpito.

Ametoa ushauri huo leo Jumapili akihubiri wakati wa misa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Minaramiwili ambayo imehudhuriwa na Rais Magufuli.

Askofu Shao amesema hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli za kupambana na rushwa, kupigania rasilimali za Watanzania, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji, kukabiliana na wizi na ubadhilifu wa mali za umma na kubana matumizi zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.

“Hatutaweza kusema tunaimaliza rushwa wakati tunaendelea kuishi kwa kupata fedha ambazo hujazifanyia kazi, ni lazima tuishi machungu ya kuimaliza rushwa, ni lazima tuishi machungu ya kuweka uadilifu katika utendaji wetu, tusipoishi machungu hayo tutaishi dunia mbili, dunia ya rushwa na dunia ya kujenga uchumi na uadilifu wa Watanzania,” amesema.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari imesema baada ya misa kumalizika Rais Magufuli amemshukuru Askofu Shao kwa mahubiri.

Amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali inachukua hatua za kupambana na rushwa na kulinda rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi.

Rais Magufuli amesema Baba wa Taifa, Julius Nyerere ambaye jana Jumamosi iliadhimishwa miaka 18 tangu kifo chake alipiga vita rushwa na alipigania rasilimali za nchi, hivyo ametaka Watanzania wote kuungana katika juhudi hizo.

Dk Magufuli amechangia Sh1 milioni kwa ajili ya kwaya ya kanisa hilo na Sh5 milioni  kwa ajili ya maendeleo ya kanisa.

Leave A Reply