The House of Favourite Newspapers

Askofu Kakobe Aanika Wakristo Wanavyoibiwa

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ameanika kile alichodai, jinsi baadhi ya wachungaji na mitume wanaohubiri kwa kuwaaminisha watu waamini maji, mafuta ya upako, chumvi, nk, na kusema kwamba wanawaibia watu hivyo kuitaka serikali iwakamate kwa kuwa wanadanganya. 

 

Askofu Kakobe aliyasema hayo mbele ya mwandishi wa gazeti hili la Uwazi wiki iliyopita mara baada ya kuhutubia katika uzinduzi wa Jukwaa la Kuhubiri Kristo (JKK). Alisema, siku hizi badala ya watu kuhubiriwa nguvu ya Kristo, wamekuwa wakihubiriwa nguvu ya mafuta, maji, keki, chumvi, bangili na makorokocho mbalimbali, jambo ambalo alisema siyo sahihi.

 

“Hawa ni matapeli na ndio wanaharibu ukristo na najua nikisema hivyo Rais Dk. John Magufuli anasikia sauti ya Kakobe, sasa wewe nabii wa uongo endelea na mchezo huo, utapigwa pingu,” alisema Askofu Kakobe.

Akaongeza: “Tumechoshwa na matapeli kuishi Tanzania, tusiruhusu matapeli katika nchi hii, tunataka kusikia manabii hawa wa uongo wakifikishwa mahakamani.

 

“Watu wanatapeliwa na wengine wanaumizwa, wanafilisiwa kwa kutapeliwa kwa jina la Ukristo na kwa jina la dini, jambo ambalo haliwezi kufumbiwa macho. “Kenya walifanya hivyo na mtu mmoja (anamtaja jina) alikamatwa na akafungwa miaka miwili jela, hawakutaka utapeli wake.

 

“Mwaka 2010 nilikwenda Kinshasa DR Kongo na tulifanya mkutano kwenye Uwanja wa Stade Des Martyrs, wakaja watu wakawa wanaangalia ile miujiza bila kutumia maji na wengi walikuwa wakizungumza Kilingala. Akaja nabii mmoja maarufu sana kule, akaniambia mtumishi hawa wote waliokuja nawafahamu.

 

“Najua hawakujui lakini kwa jinsi ulivyowaombea na kupata miujiza yao, imenishangaza sana. Ikasababisha Jumapili moja nikatembezwa katika makanisa mengi karibu kumi, tulimhubiri Yesu Kristo na si mafuta, chumvi au maji,” alisema Askofu Kakobe.

Mtumishi huyo alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kuingilia unabii huo wa kutumia mafuta, maji, chumvi, keki, stika nk ambao alidai ni wa uongo ili wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.

“Mkuu wetu wa mkoa, Paul Makonda rafiki yangu, wewe umekuwa unasimama upande wa Bwana, umefanya kazi nzuri za heshima nakukabidhi hii kazi, kamata manabii (wa uongo), tunataka kuona manabii hao wanafikishwa mahakamani,” alisema Askofu Kakobe.

Hata hivyo, Askofu Kakobe alisema yeye na wenzake, Askofu Sylvester Gamanywa wa Wapo Mission International na Mtume Vernom Fernandes wa Agape Life Church International wameamua kukemea tabia ya baadhi ya wachungaji, manabii na mitume kwa sababu wanaona mwelekeo wao ni wa hatari kwa Ukristo.

“Sisi ikitokea mtu anauza maji ya ubatizo tutamkemea, hatuwezi kumvumilia,” alisema Askofu Kakobe. Hata hivyo, baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walisema kuna baadhi ya wachungaji na manabii ambao huwatoza watu kiasi fulani cha fedha ili waombewe.

“Ni kweli kuna baadhi ya manabii na mitume ili upate huduma yao ni lazima ulipie kiasi fulani cha fedha. “Wapo ambao hutoza shilingi elfu tano na wengine hutoza shilingi laki moja na nusu, bila kutoa kiasi hicho cha fedha, huwezi kuombewa,” alisema Fidea Malimbo.

Naye Charles John mkazi wa Masaki alisema ipo haja ya watu wanaokwenda kwenye maombi kujitafakari kwa sababu siyo kawaida kwa watumishi wa Mungu kutaja kiasi cha fedha ili uombewe na tatizo lako liishe.

“Ni ukweli kwamba wengine wanatumia matatizo ya watu wanaokwenda katika makanisa yao, kujitajirisha kwa kuwatoza fedha huku wakidai kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya gharama za fomu wanazopewa kujiandikishia, jamani fomu fedha zote hizo?” alihoji John Emmanuel mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, alipozungumza na mwandishi wetu.

Hata hivyo mwanamke mmoja, Feisi Zabron, mkazi wa Tegeta alisema kuna wengine wanaombewa na kupona matatizo yao hasa kama ni ugonjwa na ukaenda kwa imani.

“Lakini kiukweli wahubiri wengi siku hizi hawahubiri ufalme wa mbinguni na badala yake huhubiri utajiri wa kupata fedha nyingi, nyumba nzuri, gari na hata kuolewa au kuoa. Kwamba ukinywa maji wanayotoa, hayo utayapata kiulaini, kitu ambacho kinatia wasiwasi na kibaya zaidi maji yenyewe wanauza bei kubwa kuliko hata yanavyouzwa mitaani,” alisema Feisi.

Wimbi kubwa la watu bila kujali dini zao siku hizi wameaminishwa na baadhi ya watu wanaojiita wachungaji, mitume na manabii kuamini katika maji, mafuta, keki, stika nk, kwamba vinaweza kukuponya maradhi au kukuondolea matatizo yako ukiamini, jambo ambalo wengi wamekuwa wakikimbilia huko kwenye makanisa yao.

Hata hivyo uchunguzi umeonesha kuwa kuna baadhi ya watu ambao wameondokana na matatizo yao baada ya kushiriki kwenye maombi ya baadhi wachungaji wanaotumia mafuta na zana nyingine.

Aidha, mbali na hilo kuna watu ambao wameshatumia fedha nyingi kwa wachungaji lakini bado matatizo yao hayajaisha. “Yaani humu ndani imekuwa shida, nimekuwa kama naishi na teja, fedha nyingi mke wangu anapeleka kanisani anakodai kuombewa.

“Wakati mwingi yuko radhi hata kuchukua fedha ya chakula, sasa nimekuwa najiuliza ni kanisa kani hilo ambalo linataka hela kila siku?” alihoji mzee mmoja aliyejitambusha kwa jina la Masuguliko mkazi wa Ukonga. Hata hivyo, mwandishi wetu alimtafuta mmoja wa wachungaji wanaotumia mafuta na maji kutibu wagonjwa ambaye jina lake tunalihifadhi na kumuuliza kuhusu huduma yake ambapo alisema:

“Ukisikia mchungaji anaita huduma ya mwenzake ni mbaya lazima naye umuulize ya kwake ina uzuri gani maana kama ni kuombea wote tuonaombea kwa njia tofauti na wagonjwa wengine wanapona na wengine hawaponi kulingana na imani zao. “Kama ni matumizi ya Biblia hata mimi natumia maandiko, kwani Yesu hakuwahi kuponya kipofu kwa kutumia mate yake?” alimaliza kwa kuhoji mchungaji huyo.

Comments are closed.