The House of Favourite Newspapers

Askofu Nkwande Akemea Uchawi, Ushoga Na Utoaji Mimba

ASKOFU MKUU wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Renatus Nkwande ameshutumu vikali uchawi, ushoga na utoaji wa mimba.

 

Ameyasema maneno hayo jana (Jumapili, Mei 12, 2019) wakati akitoa shukrani kwenye ibada ya kumsimika kuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo iliyofanyika kwenye viwanja wa Kawekamo jijini Mwanza.

 

Alisisitiza kwamba husikitika kila anaposikia watu wanaongelea mambo ya uchawi na kusema kwamba huo ni ushamba wa elimu ambapo mtu akivimba tumbo watu wanasema amerogwa na tena huwataja watu kwamba ndiyo wachawi wanaosababisha magonjwa.

 

“Huo ni ushamba wa elimu na tena huko ni kukosa imani na kushindwa kumuamini Mwenyezi Mungu,” alisema na kuongeza:  “Watu wetu wana hofu mbalimbali ambazo zimewakamata tangu utoto wao. Tuwasaidie waumini hawa ili wamwamini Mungu kwamba anaokoa na anaweza kuwaponya madhila waliyonayo. Tuwasaidie watu wetu wajikomboe kielimu, wajiendeleze kwenye masomo ya fizikia, kemia na kadhalika,” amesema.

 

Alisema anashangaa tabia ya Waafrika ya kupenda kuiga mambo ya ajabu kwa vile tu yameletwa na Wazungu. “Sisi Waafrika ni watu wa ajabu tunaiga vitu visivyo na msingi. Wameleta ushoga, tunaiga! Wameleta utoaji mimba, tunaiga. Leo hii kuna taasisi zinasambaza hata vifaa vya kutolea mimba, nasi tumekaa tunaangalia tu.

 

“Wazee wetu walipoona wamechoka ukoloni, walipigana ili kupata uhuru. Leo na sisi tupiganie uhuru kwa kukataa masuala ya ushoga na utoaji mimba. Huo ni uuaji, hiyo ni dhambi. Miongoni mwetu leo wapatikane watu wa kusimamia hayo ili ukoloni huu usiendelee kutawala akili za watu wetu,” amesema.

 

Amewaomba Watanzania wamuombe Mungu awabariki, alibariki taifa la Tanzania ili yanayofanyika yawasaidie kwenda mbinguni.

 

Pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo na hatimaye kuwatoa kwenye umaskini.

 

“Tunaamini yote anayofanya ni kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema.

 

Akizungumza kwa niaba ya Rais Magufuli na mamia ya waumini na viongozi waliohudhuria ibada hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema anatambua kuwa kuwaongoza watu kiroho na kimwili ni jambo lenye uzito mkubwa. Na kwamba uteuzi wake unadhihirisha kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kumtumikia Bwana.

 

“Sisi viongozi na waumini kwa kutambua kazi nzuri uliyoifanya hadi kufikia kupata wadhifa huo tuna imani utaweza. Nakuomba upokee mzigo huo kwa matumaini na bila kusita kwani waumini wa kanisa hili wako pamoja nawe na viongozi wenzako wote tunategemea watatoa ushirikiano kwako,” alisema Majaliwa.

 

 

Mapema, akitoa salamu za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga aliwataka waumini wa Kanda ya Ziwa wawe na mshikamano na wampe ushirikiano Askofu Mkuu Nkwande.

 

“Kuweni na upendo kama Bwana Yesu alivyofundisha na pia ombeeni utumishi mwema kwa viongozi wote wa serikali na watumishi wote wenye jukumu la kuongoza watu,” alisisitiza.

 

Pia aliishukuru serikali kwa kulipa nafasi Kanisa Katoliki ya kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za jamii kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika sekta ya elimu na afya.

 

Baada ya sherehe hiyo Waziri Mkuu aliondoka jijini Mwanza  kuelekea Arusha kupokea kundi la watalii zaidi ya 200 kutoka China.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

 

Tambwe Afunguka kurogwa na Donald Ngoma

Comments are closed.