The House of Favourite Newspapers

Askofu Shoo Awaonya Viongozi, Matajiri Akemea Ubaguzi – Video

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dkt. Ferdrick Shoo amewaonya viongozi wa Tanzania na kuwataka watumie nafasi zao kuwasaidia wengine hasa wale wenye uhitaji.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 9, 2019) wakati akitoa mahubiri kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi iliyofanyika kwenye kanisa la KKKT, Usharika wa Moshi Mjini.

 

Amesema kuna watu wakipata vyeo ama utajiri kidogo tu, wanatumia nafasi zao kunyanyasa wengine na akaonya Watanzania wasiwe wepesi wa kuhukumu, kunyanyasa au kubagua wengine.

 

Amesisitiza  kwamba kuna dhambi ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba ni ile ya kubaguana na kama Watanzania wanahitaji taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu, ni vyema wakaacha kufanya hivyo.

Dhambi nyingine inayopaswa kufanyiwa toba, alisema,  ni ile ya watu wenye nafasi kuwakanyaga wengine.

 

“Ndugu zangu tukiwa na cheo, tukiwa matajiri, tukiwa na uwezo tuvitumie kuwasaidia wengine, tuache ubinafsi, tuache kiburi, tuache kujitutumua hasa kwa viongozi wa umri mdogomdogo. Kuna mahali mmefika mnajitutumua kama chatu, acheni kabisa. Naomba tuwe na unyenyekevu ndugu zangu.

 

Akimuelezea Dkt. Mengi, amesema: “Aliwahi kusema kuwa, mali na utajiri ambao Mungu amempatia siyo kwa sababu yeye ni bora kuliko wengine, bali alimpa ili awe kama bomba la kufikisha baraka kwa wengine.

 

“Leo mtu anapata vimilioni kadhaa tu anataka atembee juu ya migongo ya watu, anapata kacheo sijui ni diwani, mkuu wa mkoa au wa wilaya, halafu unaona wenzako si kitu. Tuache na tutubu; acha kiburi namuomba Mungu atujalie roho hiyo ya unyenyekevu.”

 

Wakati huohuo, akizungumza kwa niaba ya serikali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Dkt. Mengi atakumbukwa kwa kitendo chake cha kuuchukia umaskini na zaidi kwa kazi mbalimbali ambazo alishiriki.

 

“Bila shaka kila mmoja wetu ameguswa kwa namna ya kipekee na mchango wa Dkt. Mengi. Kiukweli, marehemu Dkt. Mengi, atakumbukwa kama mwanahabari, mwanaviwanda na mfanyabiashara maarufu ambaye alitumia elimu, maarifa na utajiri wake kwa ajili ya manufaa ya wote hususan watu wenye mahitaji maalum,” amesema.

 

Amewaomba wanafamilia wasimamie makampuni ambayo Dkt. Mengi aliyaanzisha na kama watakwama wasisite kuomba msaada serikalini kwani iko pamoja nao.

 

Wakati huohuo, akielezea wasifu wa baba yake, mtoto wa marehemu, Abdiel Mengi,  alisema siyo rahisi kuyazungumzia yote kwa wakati mmoja mambo ambayo yamefanywa na baba yake bali aliwashukuru waombolezaji wote, viongozi wa serikali na wafanyakazi wa makampuni ya IPP kwa upendo wao.

 

“Mambo yote aliyoyafanya naweza kumwelezea katika sifa tatu kubwa ambazo ni: Alikuwa mzalendo, mwenye uthubutu na mwenye kupenda breakthrough (ufumbuzi). Alikuwa anafikiria tofauti na wengine. Kwanza anajiuliza kwa nini nifanye jambo hili, na nifanyeje,  ilikuwa ni suala la pili,” alisema.

 

Dkt. Mengi ambaye alifariki dunia alfajiri ya Mei 2, mwaka huu akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za Kiarabu, amezikwa katika makaburi ya familia huko Nkuu Sinde – Kisereni, Machame, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro. Ameacha mke na watoto wanne.

 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MEI 9, 2019.

Comments are closed.