ASLAY KUSHUKA DAR LIVE PASAKA HII

MKALI wa Bongo Fleva aliyewahi kuunda Yamoto Band, Aslay Isihaka anatarajiwa kushuka Sikukuu ya Pasaka ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

 

Akizungumza na Showbiz, Meneja wa Dar Live, Rajabu Mteta ‘KP Mjomba’ alisema kuwa, kwa mara ya kwanza tangu Aslay afanye muziki kivyake hajawahi kushuka katika uwanja huo wa taifa wa burudani.

 

“Siyo Dar Live tu, Aslay hajawahi kufanya shoo yoyote si Temeke wala Mbagala kwa hiyo kwa mara ya kwanza atashuka Dar Live Pasaka hii na kuporomosha vibao vyake kibao kuanzia Hauna, Natamba, Totoa, Nibebe, Likizo na Kwatu hivyo niwaombe mashabiki wote mjitokeze kwa wingi kushuhudia shoo hii ya kihistoria,” alisema KP na kuongeza kuwa listi kamili ya watakaosindikizwa itatajwa hapo baadaye.

 

Naye Aslay alisema kuwa, zipo zawadi nyingi amewatayarishia mashabiki wake kwa hiyo waje kwa wingi kujionea.

“Mashabiki wote mnajua linapokuja suala la shoo huwa silembi, nitakamua live kwa kutumia vyombo hakuna cha ‘playback’ mwanzo mwisho ni burudani tu,” alisema Aslay.

 

Burudani hiyo ya kijanja itakuwa kwa mchongo wa buku 10 tu yaani 10,000 na 8,000 kwa watu 100 wa kwanza.


Loading...

Toa comment