Aslay, Msagasumu Kuondoka na Tuzo Valentine’s Day

Aslay.

 

HIT MAKER wa Ngoma ya Natamba, Aslay Isihaka pamoja na mkali wa Singeli, Seleman Jabir ‘Msagasumu wanatarajiwa kupewa tuzo maalumu ya heshima ya ufalme katika Sikukuu ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’ (Feb. 14) ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala- Zakhem jijini Dar.

Meneja na Mratibu wa Dar Live, Rajabu Mteta ‘KP Mjomba’ alisema kuwa, usiku huo ambao ni maalum kwa wapendanao, wameandaa zawadi hizo ikiwa ni maalum kwa kutambua mchango wao kwa watu wa Mbagala na Temeke kwa ujumla.

“Sote tunajua uwezo wa Aslay ulivyo juu, hakuna ngoma ambayo ameitoa ikawa mbaya tangu akiwa katika muunganiko wa Bendi ya Yamoto, kwa nini sasa asiwe tu Mfalme wa Mbagala kwa kuwa hakuna anayemfikia kimuziki kwa kanda hii.

“Tukija kwa Msagasumu naye hivyohivyo, yeye ndiye aliyeifanya Singeli ikakubalika na kila mtu hivyo mchango wake ni muhimu, tutampatia tuzo ya ufalme pia” alisema KP Mjomba na kuongeza:

“Mbali na Aslay na Msagasumu, tutakuwa pia na kundi kongwe la Taarab la Jahazi Modern huku burudani zote hizo ukizipata kwa shilingi 10,000 tu.”

 

Msaga Sumu.

Akizungumza na Full Shangwe, Aslay alisema;

“Nitawapa mashabiki wangu kile ambacho wamekimis kutoka kwangu, ninazo nyimbo nyingi hadi sasa ambazo zipo kichwani mwa mashabiki wengi kwa hiyo naamini siku hiyo tutakuwa tukiimba pamoja.

“Ukiwa na patna wako hii si ya kukosa kwani nitawaburudisha na vibao kama Marioo, Baby, Usiitie Doa, Angekuona, Hauna, Mhudumu, Natamba na vingine vingi,” alisema Aslay.

Naye Msagasumu aliwashukuru waandaaji na kusema;

“Mwanangu mwenyewe wee njoo umependeza, njoo na mtoto wako mzurimzuri uje umsikilize mkali wa Singeli na ngoma za kubembea na mwenzako.”

Full Shangwe


Loading...

Toa comment