The House of Favourite Newspapers

ATCL Yakanusha Taarifa Inayosambaa Kwenye Mitandao Kuhusu Ndege Yake Ya Boeing 787- 8

0

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ndege yake aina ya Boeing 787- 8 yenye usajili wa namba 5H-TCJ kupelekwa kwenye matengenezo makubwa yaani Check – C kabla ya kufikisha muda wake tangu inunuliwe na kutelekezwa nchini Malaysia.

Taarifa ya ATCL ya leo imebainisha kuwa Ndege yake ya B787- 8 ipo nchini Malaysia kwa ajili ya matengenezo ya lazima ya injini zake baada ya kufikisha muda wake na sio matengenezo makubwa ya Check – C.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mha. Ladislaus Matindi amesema “Matengenezo makubwa ya ndege zetu za 787 – 8 (Dreamliner) yanafanyika hapa nchini kwenye Karakana yetu ya KIMAFA iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kila baada ya miaka 3 au masaa 12,000 chochote kitakachoanza. Karakana zetu zina wataalam wenye uzoefu wa kufanya matengenezo makubwa ya ndege ya kiwango cha Check – C”.

Ameongeza kuwa tangu ndege hizi ziwasili nchini zimefanyiwa matengenezo makubwa (Check – C) mara moja ambapo kwa ndege ya kwanza iliyowasili nchini mwaka 2018 ilifanyiwa matengenezo hayo mwaka 2021 na ya pili iliyowasili mwaka 2019 ilifanyiwa matengenezo mwaka 2022, amehitimisha, Mha. Matindi.

Tatizo la ndege kukaa muda mrefu kwenye karakana, Malaysia, linatokana na uhaba wa injini za ziada ambazo zingeweza kutumika wakati injini zake zikifanyiwa matengenezo.
Ndege za Boeing 787- 8 za ATCL zinatumia injini za Kampuni ya Rolls Royce aina ya Trent 1000.

Kwa mujibu wa miongozo ya Mamlaka za Usafiri wa Anga na watengenezaji wa injini hizo, imekuwa ni lazima injini hizo kufanyiwa matengenezo makubwa (overhaul) kila baada ya miruko 1,000. Hii ni baada ya kugundulika kwa matatizo ya kisanifu (design) katika mifumo hasa ya ufuaji wa nguvu za kuendesha ndege, kwa injini nyingi za matoleo mapya.

Aidha, Matatizo haya yamesababisha kutolewa kwa miongozo maalum kuhusu uchunguzi wa injini wa mara kwa mara iwapo katika matumizi. Injini hizo zinapopelekwa kwa matengenezo zinalazimika kuzingatia foleni au zamu (slot) kutokana na idadi kubwa ya injini zinazosubiria matengenezo na hivyo kupelekea kuchukua muda mrefu kuhitimisha matengenezo yake.

Leave A Reply