DK. CHALE SIMU: +255713350084 | IJUMAA | AFYA
TATIZO la mirija ya uzazi kushindwa kufanya kazi huitwa Tubal Dysfunction , hapa ni kwamba mirija ya uzazi imeziba au imeharibika kiasi kwamba inashindwa kusafirisha mimba hadi ndani ya kizazi hali iitwayo Epithelial Dysfunction. Athari katika mfumo wa kizazi tunazozungumzia ni kuharibika kwa maumbile ya kizazi au Pelvic lesions kutokana na matatizo mbalimbali kama maambukizi ya kizazi au PID, uvimbe ndani ya kizazi na kasoro nyinginezo. Matatizo haya ya kizazi huzuia mimba kutungwa au kama imeshatungwa inashindwa kujikita kwenye mji wa mimba.
CHANZO CHA TATIZO
Mirija kushindwa kufanya kazi au kuziba hutokana na maambukizi ya muda mrefu ya kizazi au Pelvic Inflammatory Diseases au kwa kifupi PID. Chanzo kingine ni uwepo wa maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB katika viungo vya uzazi, endapo mama ana historia kwamba alishawahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo hivyo hupata makovu ya ndani na kusababisha mirija izibe.
Vilevile endapo kidole tumbo kiitwacho Appendex kitapasuka huweza kuleta athari hizo. Matatizo au athari katika mfumo wa uzazi hapa tunazungumzia mfuko wa kizazi kwa ujumla na tatizo kubwa hutokana na kusafisha kizazi mara kwa mara hasa kwa wale wanaotoa mimba au wanaoharibikiwa na mimba mara kwa mara na kufanya kila mara wawe wanasafishwa kizazi.
Hali hii ya kusafisha kizazi kila wakati huzalisha makovu ndani ya kizazi na kufanya kuta za kizazi zishikamane, tatizo hili huitwa Asherman’s Syndrome , ni kubwa na husababisha ugumba na mwanamke huwa anapoteza kupata siku zake za hedhi. Uwepo wa uvimbe wa Fibroid husababisha kuziba mirija katika kizazi na kuleta tatizo la kutoshika mimba. Kasoro za maumbile ya kizazi huchangia.
Makovu ya kizazi yaitwayo Pelvic Adhensions husababishwa na maambukizi sugu yatokanayo na magonjwa ya zinaa au kuharibika kwa mimba. Kasoro nyingine za kizazi ni tabaka la ndani la kizazi kugeuka na kuwa kwa nje, hali iitwayo Endometriosis ambapo kizazi na mirija kwa pamoja huathirika na kukusababishia kupoteza uwezo wa kushika mimba.
DALILI ZA TATIZO
Mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika ameishi mwaka mmoja anatafuta mtoto lakini hapati, siku zake za hedhi hazieleweki, analalamika maumivu chini ya tumbo kwa muda mrefu, pia wakati mwingine hupata maumivu wakati wa tendo la ndoa ingawa siyo kwa wote. Wapo wengine wanakuwa wamefunga kupata hedhi kwa muda mrefu, kutokwa na uchafu ukeni na wakati mwingine hali hiyo inaweza kuwa na muwasho au la.
UCHUNGUZI
Uchunguzi hufanyika katika kliniki za magonjwa ya akina mama kwenye hospitali za mikoa ambapo vipimo vya mirija na kizazi vitafanyika. Vipimo vya damu kujua kiwango cha vichocheo muhimu vitafanyika na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa. Historia ya mgonjwa itachunguzwa kwa kina ambapo tayari ana mtoto, mimba zimeharibika, Athari za mirija ya uzazi kushindwa kufanya kazi alishatumia uzazi wa mpango au alishawahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo uliohusisha mirija ya uzazi na endapo alishawahi kupata maambukizi ya kizazi au ukeni kwa muda mrefu.
TIBA NA USHAURI
Matibabu ni baada ya uchunguzi wa kina, tiba inaweza kuwa ni dawa, upasuaji au kuzibua mirija ya uzazi. Kama ikithibitishwa una maambukizi sugu, basi matibabu yatafanyika au kama tatizo ni vichocheo pia tiba itafanyika. Ni vizuri umuone daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi na tiba.