ATOGS Kuongoza Ujumbe Wa Tanzania Kwenye Mkutano Na Maonyesho Ya Teknolojia Marekani

Dar es Salaam 21 Aprili 2023: Jumuiya ya Watoa Huduma za Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) itaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano mkubwa na maonyesho ya teknalojia yatakayofanyika Texas nchini Marekani wiki ijayo.
Ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani hapa nchini, ATOGS iliandaa mkutano wa maandalizi kabla ya kusafiri kwa wanachama wake ambao ni wadau katika sekta za nishati, mafuta na gesi.
Mkutano huo wa maandalizi ulikuwa chini ya Mwenyekiti wa Abdulsamad Abdulrahim ATOGS na pia ulihudhuriwa na Ken Walsh ambaye ni afisa mwandamizi wa masuala ya biashara katika ubalozi wa Marekani na Andrew Mahiga ambaye ni mtaalamu wa masuala ya biashara kutoka ubalozi wa Marekani na wanachama wa ATOGS watakaosafiri.

Akizungumza muda mfupi baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa ATOGS alisema mkutano huo ulilenga kuwafahamisha taratibu mbalimbali wajumbe wataosafiri ikiwa ni pamoja na ratiba nzima ya mkutano na maonyesho hayo makubwa duniani.
Ujumbe wa Tanzania unaundwa na viongozi 9 wa sekta pamoja na maafisa watendaji wakuu. Mkutano utafanyika kuanzia tarehe 1 hadi 4 mwezi Mei mwaka huu Texas nchini Marekani.
Abdulsamad alisema ujumbe wa Tanzania utapata fursa ya kushiriki mikutano ya kielimu na ufundi kwenye mkutano huo mkubwa, na kupata fursa za kufanya mikutano na wadau mbalimbali katika sekta zao pamoja na kutengeneza fursa za ushirikiano, biashara na uwekezaji.
“Ujumbe wetu pia utaweza kukutana na mtandao wa wataalamu zaidi ya 59,000 katika sekta ya nishati kutoka nchi zaidi ya 40 watakaokuwepo katika mkutano huo. Pia zitatolewa mada na zaidi ya wazungumzaji 100 ambao wataelezea vumbuzi mbalimbali tunazozitarajia kwa miaka 50 ijayo,” alisema
Aliongeza kuwa ujumbe huo pia utapata fursa kukutana na maafisa wa ngazi za juu kutoka kwa makampuni makubwa ya uzalishaji na ugavi na kujionea vumbuzi mbalimbali za kiteknalojia.