AUAWA KWA VISU, ATUPWA BWAWANI

MWANAUME mmoja ambaye hajafahamika jina wala makazi yake ameuawa kwa visu na watu wasiojulikana kisha mwili wake kutupwa katika bwawa la maji lililopo katika Mtaa wa Shunu, Kata ya Nyahanga Wilayani Kahama mkoani Shinyanga. 

 

Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyahanga, Felician Fabi aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mwili wa mwanaume huyo uliokotwa na wasamaria wema Aprili 16 mwaka huu, saa saba mchana katika bwawa la maji lililopo katika Mtaa wa Shunu.

Mtendaji huyo alisema tukio hilo limemsikitisha na limetia doa kata yake kwa kuwa limekuja kipindi ambacho Mtaa wa Shunu una changamoto kubwa ya ulinzi shirikishi.“Kwa kweli tukio la mauaji katika Kata yangu limeshitua wengi, haijawahi kutokea, hili naweza kusema kuwa ni la mwaka. Na kwa kuwa hatambuliki, ni vyema watu wajitokeze ili waweze kumtambua kama ni ndugu yao,” alisema Felician.

 

Akizungumzia mauaji hayo, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Enock Faustine alisema kuwa anavyoona yeye matukio hayo yanatokana na baadhi ya vijana kutopenda kujishughulisha hivyo kufanya vitendo vya uporaji kwa kuua. “Ni tukio baya sana na nahisi wanaofanya hivi ni wahalifu ambao hupora na kuua, ni vyema vyombo vya usalama vikayatolea macho matukio ya sampuli hii,” alisema Enock.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao alikiri kupokea taarifa za tukio hilo na kufafanua kuwa chanzo ni wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuongeza kuwa japokuwa bado hakuna mwananchi yoyote anayeshikiliwa kuhusika moja kwa moja na mauaji hayo, watakaokamatwa sheria itachukua mkondo wake.

 

Kamanda Abwao alisema kwa sasa ametuma kikosi kazi kutoka Shinyanga kwenda Kahama kuongeza nguvu ili kuwasaka na kuwabaini watu wote waliohusika na tukio la mauaji ya mwananchi huyo.

 

Abwao aliagiza kuwa wahalifu wakikamatwa wafikishwe katika vyombo vya sheria ama kituo cha Polisi wakiwa wazima ili wapate fursa ya kuhojiwa, hali ambayo itasaidia kuupata mnyororo mzima wa waharifu. Mwili wa mwanaume huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa ajili ya utambuzi.

JAMAA Aliyejifanya ‘MCHUNGAJI’ Alivyokamatwa na Madawa DAR!


Loading...

Toa comment