Aucho, Bangala Waweka Rekodi Mpya Bara

 

MAJEMBE mapya ndani ya Yanga yanayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi raia wa Tunisia, Khalid Aucho ambaye ni kiungo na Yannick Bangala ambaye ni beki wameshindikana Bongo kutokana na rekodi zao kuwa matata kila wawapo ndani ya uwanja.

 

Nyota hao wawili kwenye mechi mbili za ligi wameweza kutumia dakika 180 kwa kuwa walipoanza Nabi hakuweza kuwafanyia mabadiliko kutokana na kukubali uwezo wa nyota hao na pia timu ya Yanga haijafungwa kwenye mechi mbili za ligi ambazo wamecheza.

 

Ilikuwa ni kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambapo Yanga ilishinda bao 1-0 na bao lilifungwa na mzawa Feisal Salum ambapo Bangala na Aucho waliweza kuwadhibiti vijana wa Francis Baraza na kuweka rekodi ya kuanza mchezo wao wa kwanza bila kuruhusu bao tofauti na msimu wa 2020/21, walipolazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Tanzania Prisons.

 

Pia kwenye mchezo wa pili, mbele ya Kagera Sugar miamba hiyo iliweza kuonyesha kazi baada ya kuwa ni mhimili wa timu ya Yanga kwa kuwa mashambulizi yote yalianza kujengwa kupitia kwa Bangala pamoja na Aucho ambaye alikuwa na kazi ya kusambaza pasi kwa wachezaji wa Yanga.

 

Hata bao la Yanga ambalo lilifungwa na Jesus Moloko dakika ya 16 mbele ya Geita Gold kazi ilianza kwenye miguu ya Bangala aliyempa pasi Kibwana Shomari aliyempa pasi Yacouba Songne aliyetoa pasi yake ya kwanza ya bao kwa msimu wa 2021/22.

 

Rekodi zinaonyesha kuwa Bangala alipiga jumla ya pasi 98, mbele ya Geita Gold juzi na aliweza kuwa na utulivu na hali ya kujiamini hali iliyofanya akaweza kukokota mipira mara 17.

 

Kwa upande wa Aucho yeye alipiga jumla ya pasi 65, aliweza kukokota mipira mara 12 huku akichezewa faulo mara 9 na wana Geita Gold wanaonolewa na Kocha Mkuu, Ettiene Ndayiragije.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Mkuu wa Yanga, Nabi alisema kuwa anafurahishwa na uwezo wa wachezaji hao na anapenda kuona wote wakicheza ili kupata kile ambacho wanakihitaji.

 

“Ninapenda kuona namna ambavyo Bangala anacheza iwe ni Aucho ama Job, kikubwa nahitaji kuona wote wanacheza na uwezo wao ni mkubwa kwa kuwa ninawajua na nipo nao,” alisema Nabi.3473
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment