The House of Favourite Newspapers

Aunt Aanika Siri Kumrudia Iyobo

KUNA usemi usemao bibi na bwana wakigombana, shika jembe ukalime! Hilo limedhihirika baada ya tukio la hivi karibuni la staa wa filamu Bongo, Aunt Ezekiel kurudiana na mzazi mwenziye, Moze Iyobo. 

 

Wawili hao walitangaza kurudiana juzikati kwenye ‘bethdei’ ya Aunt iliyofanyika ndani ya baa yake ya The Luxe iliyopo Mikocheni jijini Dar baada ya kuwa mbalimbali kwa muda mrefu.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Aunt alisema watu wanaweza kuhoji kilichomfanya arudishe majeshi kwa dansa huyo wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond’ lakini ukweli ni kwamba, siri ni umuhimu wa baba katika familia.

Alisema kwa kuwa walishajaaliwa mtoto mmoja, Cookie ilikuwa ni ngumu sana kumfanya mtoto huyo awe na furaha wakati hapati malezi ya wazazi wake wawili. Aunt alisema, alikuwa akiona wazi kuwa mwanaye hana furaha kutokana na uhusiano wao kuvunjika, hivyo akaona kwa faida ya mtoto, wasahau yaliyopita ili wagange yajayo.

 

“Watu watambue kuwa yule ni mzazi mwenzangu kwa hiyo kufanya vile wasishtuke maana sisi tumeshazaa na ninampenda mtoto wangu na ninapenda nimuone ana furaha.

“Ndiyo maana nikaona itakuwa ni jambo la busara kurudiana kwa manufaa mapana ya mtoto wetu,” alisema Aunt. Awali, Aunt na Moze walizinguana na kuamua kila mmoja achukue hamsini zake ambapo Moze aliwahi kudaiwa kuhamia kwa mwanamke mwingine huku Aunt naye akijiweka kwa mwanaume aliyefahamika kwa jina la Alfo.

 

Alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na mwanaume huyo baada ya kusema amerudi kwa Iyobo, muigizaji huyo alisema waliachana muda mrefu kimyakimya na ndiyo maana hata zile mbwembwe za mitandaoni zikawa hazionekani.

 

Wakizungumzia uamuzi wa Aunt kurudi kwa Iyobo, baadhi ya mashabiki wa mastaa hao walisema kuwa, ilikuwa ni ngumu kuachana mazima kwani walionekana kuwa na mapenzi ya dhati.

“Unajua Aunt na Iyobo walikuwa wakipendana ukweli, ndiyo maana walipoachana nilijua ipo siku watarudiana,” alisema Sesy wa Sinza jijini Dar na kuongeza: “Nilikuwa naipenda sana hii kapo, nilikuwa nikiomba kila siku warudiane, hatimaye yametimia.”

STORI: IMELDA MTEMA, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.