Aussems: Nawaonea Huruma Horoya Kwa Kitakachowakuta
KOCHA wa zamani wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ameweka bayana kuwa haoni namna yoyote ya wapinzani wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Horoya kuweza kutoka salama kwenye Uwanja wa Mkapa kutokana wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa morali kubwa katika mechi za maamuzi.
Simba ambao wanakamata nafasi ya pili katika msimamo kundi C wakiwa na pointi 6 wakati vinara wa kundi hilo Raja Casablanca wenye alama 12 baada ya timu zote kucheza mechi 4. Mechi ya kwanza Horoya alishinda 1-0 Simba.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Aussems licha ya Simba ya msimu huu kuonekana nyepesi lakini haoni urahisi wa Horoya kupata matokeo yoyote ya ushindi kwa kuwa Simba wanatambua ukubwa wa mchezo huo utakaowasaidia kuweza kupata hesabu nzuri ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
“Ni ngumu sana kwangu kufuatilia timu ambayo kwa sasa sipo nayo lakini sioni nafasi ya Horoya kuweza kuweza kupata ushindi au sare na Simba ikiwa ikiwa inacheza kwa Mkapa kwa sababu ni moja kati ya timu ambazo wachezaji wake wanajitoa kuweza kufikia malengo.
“Nakumbuka tulivyocheza na Nkana pamoja na AS Vita katika mechi ambazo ziliamua hatima yetu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana morali ya wachezaji ilivyokuwa kubwa kitu ambacho naona kinaenda kutokea katika mchezo na Horoya, binafsi nawatakia ushindi Simba ili waende robo fainali,” alisema Aussems.