Aussems: Tukutane Machinjioni

IKICHEZA kwa kujiamini na mbinu za hali ya juu, juzi Jumamosi Simba ililazimisha suluhu ugenini dhidi ya wenyeji, UD Songo ya Msumbiji. Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Beira, Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisisitiza kwamba; “Tunakwenda kumaliza kazi Dar.”

 

Simba iliandika rekodi ndani ya msimu mpya baada ya kutoruhusu bao lolote ikianzia mashindano hayo makubwa ugenini. Msimu uliopita kwenye hatua ya awali Simba ilianzia nyumbani dhidi ya Mbabane ikashinda 4-1, ugenini ikashinda mabao 4-0.

 

Baada ya hapo katika mechi zote ilizocheza ugenini ikaruhusu mabao mengi. Katika mchezo wa jana Simba ilionekana kucheza kwa kujiamini huku safu ya ulinzi ikifanya kazi ya ziada.

 

Ndani ya dakika 45 za kwanza Simba ilipiga mashuti matatu ambayo hayakuwa
na madhara lakini mengine mawili nusura yawaamshe mashabiki kwani kipa alipangua yakawa kona.

 

Wekundu hao walipata kona nne za haraka huku wakionekana kutawala zaidi eneo la katikati na kuwalazimisha wenyeji kupiga pasi ndefu ambazo hata hivyo walionyesha udhaifu mkubwa kwenye umaliziaji kwani walikuwa wakipaisha au kupiga pasi fyongo
ambazo zilikuwa mboga kwa Benno Kakolanya.

 

UD Songo walicheza mpira wa kuvizia kipindi cha pili lakini wakadhibitiwa na Nyoni na Wawa ambao walionekana kujiamini. Shiboub ambaye ni raia wa Sudan katika mechi jana alitawala kiungo na kuziba mianya mingi ya wenyeji kuwafikia mabeki wa Simba.

 

Mkude muda mwingi alikuwa akiinasa mipira, kuidhibiti na kumpa Chama ambaye kazi yake ilikuwa kusambaza tu. Kwa mujibu wa kocha na viongozi wa Simba, uwanja uliochezwa mechi hiyo wa Campo Do Ferroviario Da Beira ulikuwa chakavu sana na haukuruhusu kucheza kiwango chao ingawa suluhu bado inawabeba.

 

Aussems alisisitiza kwamba wana nafasi kubwa ya kushinda Dar es Salaam kwenye mechi ya marudiano na kusonga mbele na hawana wasiwasi.

 

“Ulikuwa mchezo wa wazi, walikuwa wakijaribu kufunga na kwetu ilikuwa hivyo, jambo muhimu hatujaruhusu goli. Mchezo wa marudiano utakaochezwa Dar ni muhimu, kwa ushangiliaji wa mashabiki wetu na uwanja mzuri nafikiri tutafanya vizuri,” alisema Kocha Aussems.


Loading...

Toa comment