The House of Favourite Newspapers

Aveva: Ajib, Kessy wametuhujumu

0

aveva.jpgWilbert Molandi, Dar es salaam

BAADA ya kuukosa Ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, uongozi wa Simba umewataja beki wa pembeni, Hassan Kessy na Ibrahim Ajib kuwa ndiyo waliosababisha wao walikose taji hilo.

Kauli hiyo, ilitolewa jana na rais wa timu hiyo, Evans Aveva  alipokuwa akizungumza kwenye Hotel ya Colosseum iliyopo Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Simba wamelikosa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo ambapo mara ya mwisho kulichukua ilikuwa ni msimu wa 2011/2012, kabla ya msimu wa 2012/2013 kuchukuliwa na Yanga, Azam FC (2013/2014), Yanga  (2014/2015), Yanga (2015/2016).

Akizungumza na Championi Jumatano, Aveva alisema kwanza anawaomba radhi mashabiki wa Simba kwa kushindwa kufikia malengo yao waliyoyaahidi wakati wanaingia madarakani mwaka 2014 ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu na Kombe la FA huku akizitaja sababu ambazo ni;

Usaliti; “Sababu ya kwanza iliyosababisha kutotwaa taji hilo la ligi kuu msimu huu ni usaliti uliofanywa na Kessy aliyecheza rafu ya makusudi na kutolewa kwa kadi nyekundu mechi na Toto Africans ambayo tulihitaji ushindi na baada ya siku chache tukapata taarifa kuwa amesaini Yanga

“Hiyo ikatokea kwa Ajib ambaye naye alimchezea rafu ya makusudi mchezaji wa Mwadui FC na kutolewa nje ya uwanja wakati timu ikihitaji ushindi kwenye mchezo huo na baadaye usiku kutuma meseji kwa viongozi akiwaaga kuwa anakwenda Afrika Kusini kwenye majaribio.

Wachezaji kushinikiza mgomo; “Wakati tunajiandaa na mechi dhidi ya Majimaji, kabla ya kuanza safari ya kwenda Songea, wachezaji Kiiza (Hamisi), Juuko (Murshid), Nimuboma (Emiry) waliwashinikiza wenzao wa kimataifa Angban (Vincent) na Majabvi (Justice) kutokwenda kwenye mechi hiyo hadi watakapolipwa mishahara yao.

Ushindani; “Hii nayo ni sababu kubwa iliyochangia timu kufanya vibaya, kiukweli ushindani umeongezeka kwa kiasi kikubwa, mwanzoni tulikuwa tukijiandaa na ligi kuu kwa kuihofia Yanga, lakini sasa hivi ushindani umeongezeka baada ya zile timu ndogo nazo kupata udhamini.

TFF; “Utendaji mzima wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nao umechangia sisi tufanye vibaya kutokana na upangaji wao mbaya wa ratiba ambayo inachangamoto kubwa, hivyo TFF inatakiwa kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Waamuzi; “Mwamuzi wa mechi ya Simba na Yanga, Jonesia Rukyaa ambaye alichezesha mechi yetu ya mwisho dhidi ya hao watani wetu naye alichangia kutokana kuchezesha mechi hiyo kwa kuegemea sehemu moja, hiyo ni changamoto kwa TFF kuleta waamuzi kutoka nje kila inayotukutanisha na Yanga ambayo ni ‘derby’,” alisema Aveva.

Mara baada ya kumaliza sababu hizo zilizowanyima ubingwa, Aveva aliongeza kuwa kwa sasa klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa uwanja wake uliopo Bunju.

Aliongeza kuwa uongozi upo kwenye hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa uwanja huo utakaogharimu shilingi Bilioni 3.2.

Pia wamepanga msimu ujao kuwa na benchi bora la ufundi ili kuhakikisha wanafanya vizuri msimu huo na kutwaa makombe.

Leave A Reply