AWAMU 5 ZA URAIS NA MAISHA YA WABONGO

HISTORIA ya nchi yetu imejengwa na awamu tano za urais, ukiweka kando tawala la kimila na kikoloni, awamu hizi zinaambatana na hali ya maisha ya watu yalivyokuwa.

Pengine kinachotajwa kushangaza wengi ni mpangilio usio rasmi wa tabia za marais waliongoza Tanzania, kwamba akiongoza mkali anayefuata anakuwa mpole.

Hicho ni kinogesho lakini hoja ni urahisi wa hali ya maisha ya watu yalivyo katika awamu hizi tano za uongozi wa nchi.

 

Maana mitaani zipo kauli “Bora enzi za Mwinyi maisha yalikuwa rahisi.”

Wengine “huyu aliyepo ni bora kuliko aliyepita” na mambo kama hayo. Nia ya makala haya japo si kwa undani sana ni kujaribu kuelezea nini kilifanyika katika awamu hizi za uongozi, lengo ni kuwekana sawa mahali tusipopajua au tuliposahau.

JULIUS NYERERE Awamu: Ya Kwanza. Kuzaliwa: Aprili 13, 1922 Kuongoza: 1961-1985 Tabia: Mkali.

AWAMU YA KWANZA

Hii ilikuwa ni awamu ya kujenga misingi ya nchi, kuwatoa watu katika mawazo ya kutawaliwa na wakoloni na kuwajengea taswira mpya ya kujitawala.

Mbali na hilo uongozi wa Nyerere ulipambana pia kujenga uchumi wa nchi katika mazingira ya kujitawa; mwelekeo ulikuwa ni KUJITEGEMEA.

Tangu uhuru mwaka 1961 hadi mwanzoni mwa miaka ya 70, hali za watu kimaisha hazikutabirika kwa sababu watu waliishi na kumbukumbu za kikoloni.

Mabakibaki ya miundombinu, barabara na huduma za afya, maji umeme na maji yalikuwa ya kikolonikoloni, kiasi kwamba watu hawakuona tofauti kubwa ya kimaisha.

 

Hii ni kwa mujibu wa mahojiano kati ya makala haya na wazee mbalimbali waliokuwepo enzi hizo.

Inaelezwa kwamba hata mawazo ya Nyerere yalikuwa ni kulijenga taifa katika msingi uliojengwa kikoloni, Tanzania ilijikita zaidi katika uchumi wa viwanda.

Itakumbukwa kuwa katika miaka ya 70 hadi 80 Tanzania ilikuwa na viwanda lukuki vya kusindika nyama, kutengeneza viatu, nguo, ngozi na kuunganisha magari redio nakadhalika.

Hata hivyo, kiongozi wa wakati huo hakuona kama ukombozi wa kiuchumi ungeweza kufanikiwa kwa kuwa na viwanda peke yake bila kukuza uzalishaji wa malighafi zitakazotumika viwandani.

 

Sera ya Ujamaa na Kujitegemea ikapewa nguvu. Kuanzia mwaka 1970-1974 mkakati wa kuanzisha vijiji vya ujamaa uliwekwa na lengo ni kuwatawanya watu maeneo mbalimbali yenye nafasi wakazalishe mazao.

Opareshi kubwa ya kuhamia vijijini ilifanywa mwaka 1974 ambapo watu walihamishwa kutoka kwenye makazi yao na kuhamishiwa porini kuanzisha vijiji vipya.

Hali ya maisha ya watu kipindi hicho inatajwa kuyumba, shida kubwa ilitokea kwa sababu wingi kati ya waliohamishwa walipelekwa mahali ambako hakukuwa na huduma za kijamii.

 

Mzee Hamis Juma mkazi wa Uyui Tabora, anasema nyakati hizo walilazimika kutumia magome ya miti yenye povu na mipapai kufulia nguo kama mbadala wa sabuni.

Wazee wa enzi hizo walichimba chumvi kwenye udogo wenye chumvichumvi na kusindika magadi kisha kupata ladha ya chumvi iliyotumika kuungia vyakula.

Maisha ya watu yaliyumba, nchi iliingia katika misukosuko mingi, wahujumu uchumi walitumia shida za watu kujinufaisha; sabuni, chumvi vililanguliwa na kuuzwa kwa bei kubwa ambayo mtu wa kawaida hakumudu kuvinunua.

 

Serikali ikalazimika kusimamia biashara hasa za mahitaji muhimu ili kulinda hali za wananchi. Ni kama Nyerere alisema hawezi kukubali kushindwa na wahujumu uchumi.

Baadaye kidogo hali ya nchi iliimarika; maisha ya watu katika vijiji vilivyoanzishwa yaliboreka; uzalishaji mazao ulikuwa mkubwa; vijijini kukawa sehemu ya raha kuishi.

Enzi hizo kukaa mjini kuliwahusu matarishi na wafanyakazi kwenye taasisi za umma na viwandani vijana wengi waliishi vijijini.

Mtikisiko mkubwa wa mafanikio yaliyoletwa na sera ya Ujamaa yanatajwa kusababishwa na nchi kuingia kwenye vita na Uganda kati ya mwaka 1978-1979.

 

Wazee wanasema licha ya Tanzania kushinda kwa kishindo vita hiyo lakini inadaiwa ilijichimbia kaburi la umaskini wa kutupwa kwani tangu kumalizika kwa vita hivyo mambo hayakwenda vizuri tena.

Vitu vilipanda bei na vilikuwa havipatikani, ulanguzi wa bidhaa uliingia na kupigwa marufuku, haikuruhusiwa mtu binafsi kutembeza sigara au pipi mkononi, ukipatika kifungo cha kuhujumu uchumi kilikuita.

Kama hiyo haitoshi viwanda vingi vilianza kuzorota, maisha ya mjini yakawa moto na vijijini nako watu waliishi kwa kuvumilia kwa vile hakukuwa na cha kufanya.

ALI H. MWINYI Awamu: Ya Pili. Kuzaliwa: Mei 8, 1925 Kuongoza: 1985-1995 Tabia: Mpole.

AWAMU YA PILI

Alipoingia Rais Ali Hassan Mwinyi kushika nafasi ya Nyerere baada ya kung’atuka alikutana na mkwamo wa bidhaa mitaani, akageuza kimyakimya sera ya Ujamaa aliyoiacha mwalimu na kuanzisha mfumo mpya aliouita ruksa.

Mwinyi hakuona haja ya kuzuia watu wasiagize nguo, chumvi, sukari na bidhaa nyingine wakati Serikali inayozuia watu wasifanye hivyo haina uwezo.

 

Kama wamachinga wanafurahia maisha yao mitaani leo hii na biashara zao za kutembeza basi wasilale bila kumumbea heri mzee Mwinyi, huyo ndiye aliyeleta soko huria na ruksa ya mtu kufanya biashara popote. Kama hilo halitoshi awamu hii ndiyo ilianzisha pia mambo ya vyama vingi, hivyo kwa wenye demokrasia zao wasisite kumpa saluti Mwingi.

Maisha ya watu kipindi chake yalikuwa mazuri kwa sababu fedha ilikuwepo mifukoni mwa wananchi, lakini wachambuzi wa mambo wanasema Serikali ilikuwa haina fedha.

Kuna tatizo gani kiuchumi? Si nia ya makala haya kueleza haya lakini itoshe kusema wakati wa Mwinyi ujenzi wa nyumba bora, uanzishwaji wa maduka mitaani na harakati za kujitafutia fedha ndipo ulipoanzia.

BENJAMIN MKAPA Awamu: Ya Tatu. Kuzaliwa: Novemba 12, 1938. Kuongoza:1995-2005 Tabia: Mkali.

AWAMU YA TATU

Baada ya Mwinyi kuondoka Ikulu, akafuata Rais Benjamini Wiliam Mkapa; alipoingia madarakani alikuta soko huria, yeye akasema linaweza kuwepo soko huria lakini uwepo wake uambatane na ulipaji kodi.

Mbali na hilo akafungua milango ya wawekezaji ambao alilenga waje kufufua viwanda vilivyokufa na kuinua uchumi uliodorola.

 

Hali ya maisha ya watu ikawa ngumu kwa sababu ya uthibiti mapato uliochukuliwa, watu mitaani wakaanza kupiga kilele hali imekuwa ngumu.

Wengine walifika mbali kwa kuiita hali ya maisha wakati huo ni UKAPA, lakini Mkapa mwenye jina lake akasema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, akimaanisha maisha ya ujanjaujanja haukuwa wakati wake.

JAKAYA KIKWETE Awamu: Ya Nne. Kuzaliwa: Oktoba 7, 1950. Kuongoza: 2005-2015. Tabia: Mpole.

AWAMU YA NNE

Awamu hii iliingia na kaulimbiu ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Harakati nyingi za kutafua maisha hazikuwekewa vizingiti. Rais wake alikuwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Mambo yakawa mepesi, mapedeshee wakashika miji, wakatesa kwenye kumbi mbalimbali za starehe; fedha kila mtu alikuwa nayo pengine swali la kuulizana lilikuwa: Una mkwanja wa maana?

Basi vijana wa leo wanasema mitaani maisha yakawa ni kula bata na kutambiana: “ Unanijua mimi nani?”

JOHN MAGUFULI Awamu: Tano. Kuzaliwa: Oktoba 29, 1959. Kuongoza 2015-sasa Tabia: Mkali.

AWAMU YA TANO

Wakati anamfanyia kampeni ili achukue kijiti cha urais aliwaambia wananchi ‘mlisema mimi mpole sasa nimewaletea chuma hiki’ akimaanisha Rais wa sasa Magufuli.

Hata Rais Magufuli alipotangazwa mshindi wa kiti cha urais, wakati akiwashukuru wananchi, katika Ofisi za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Kikwete alirudia maneno yake yaleyale:

“Nimeondoka miye, tumeleta chuma hiki. Pale nilipochoka miye, yeye atakwenda kwa kasi zaidi. Yeye ana nguvu kuliko miye… na mlikuwa mnasema mimi mpolempole, sasa mabadiliko kuweka mkali. Na ameanza kutema cheche.”

 

Magufuli aliposhika nchi akaleta sera ya Tanzania ya Viwanda watu wakasema ‘Nyerere kafufuka’ kwa sura yake maana ni kama anapita kulekule alikopita kiongozi wa Awamu ya Kwanza.

Lakini kadiri siku zinavyokwenda ni kama watu wanasema huyu aliyepo hivi sasa ni zaidi ya Nyerere. Maisha ya watu hasa wasiofanya kazi yanaonekana kuwa magumu kwa sababu misheni town siku hizi fyekelea mbali, ujanjaujanja wa kutembea na suti huku unatisha watu umetoweka sasa hivi HAPA KAZI TU!

 

Na kazi yenyewe iwe halali. Aidha katika hali inayoonesha kuwa ni ya matumaini kwa maisha ya Watanzania wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema awamu hii inapita njia sahihi katika kukuza uchumi.

 

Maana katika kipindi kifupi tayari Serikali imeweza kufufua shirika la ndege, kujenga reli ya kisasa, kutoa elimu bure, kupambana na ufisadi wa mali ya umma na kujenga nidhamu ya utumishi ambapo leo hii watu wanapiga kazi kila sekta.

MAKALA: RICHARD MANYOTA, UWAZI

Kauli ‘TATA’ za Rais MAGUFULI Zilizotikisa 2018!


Loading...

Toa comment