The House of Favourite Newspapers

AY Alivyopenya Kwenye Corona

0

 

“Dan’Hela

inaonesha kabisa hupendi watu

Sogea…(karibu)

Bila wewe jua Maisha si kitu

Dan’Hela…Ooh Ooh!

Inaonesha kabisa hupendi watu

Usijepotea… (Dan’Hela)

Bila wewe jua Maisha si kitu hayaya!”

 

HII ni korasi tamu ya Ngoma ya Dan’Hela kutoka kwa lejendari wa Hip Hop Bongo, Ambwene Allen Yessayah almaarufu AY.

AY au Mzee wa Komesho hahitaji utambulisho mreefu kwani anafahamika Bongo, Afrika Mashariki, Afrika na kwingineko duniani.

AY ni miongoni mwa wanamuziki wakongwe wa Bongo Fleva waliotengeneza tundu ambalo limepitisha vijana wengi na kujikuta wakifaidi matunda ya muziki huu.

 

AY amesikika kwenye ngoma kibao kwa zaidi ya miaka 20 kwenye Bongo Fleva tangu enzi za East Coast Team hadi leo.

Baadhi ya ngoma za AY zilizosikika zaidi na bado zinasikika ni pamoja na zile zinazopatikana kwenye albam zake za Raha Kamili (2003), Hisia Zangu (2005) na Habari Ndiyo Hiyo (2008). Nje ya albam hizo kuna ngoma nyingine kama Zigo.

 

KINGS & QUEENS

Microphone, More & More, Touch Me, Yule, Zigo Remix na nyingine kibao huku akitajwa kuwa kinara wa kolabo na wasanii wakubwa wa nje ya Bongo. Kuhusu tuzo, zipo kibao kabatini kiasi kwamba tukianza kuzitaja hapa hapatatosha.

 

Mbali na muziki, AY ni mjasiriamali, mwigizaji, prodyuza, mwanamitindo na baba wa familia.

Tangu kuanza mwaka huu wa 2020, OVER ZE WEEKEND haikupata nafasi ya kupiga stori na AY ambaye ameachia ngoma yake mpya ya Dan’Hela katikati ya janga la maambukizi ya Virusi vya Corona, lakini ikapenya na bado mashairi, midundo na melodi zake zinasikika kwenye playlist mbalimbali za online na mainstream.

 

OVER ZE WEEKEND inakuletea mahojiano maalum (exclusive) na AY ambaye anafunguka kuhusu ngoma yake hiyo mpya na ishu mbalimbali zilizotrendi kuhusu yeye. Dondoka naye;

OVER ZE WEEKEND: AY ngoma yako ya Dan’hela bado inasikika pamoja na kwamba umeiachia katikati ya janga la Corona na kuna wasanii wengine wameachia ngoma zao. Je, nini siri ya mafanikio?

 

AY: Nafikiri ni mapenzi waliyonayo mashabiki wangu ambao ndiyo hunisababisha kufanya vizuri kwa sababu huwa nakaa na kujiuliza niwape ladha gani ambayo wataifurahia. Nikipata jibu ndiyo naachia ngoma na inafanya vizuri. Kwa hiyo ni watu ambao wana mapenzi ya dhati juu ya muziki wetu ndiyo ambao wananifanya nifanye vizuri wakati wote.

 

OVER ZE WEEKEND: AY wewe ni miongoni mwa wasanii ambao huzunguka duniani kwa ajili ya kufanya shoo, lakini kwa sasa dunia imekumbwa na janga la Corona. Je, imekuathiri kiasi gani?

 

AY: Siyo mimi tu niliyeathirika, ni kila mtu na kila mahali. Ni kweli mara nyingi huwa nakwenda nje kupiga shoo, lakini sasa hivi kila kitu kimeharibika. Hata kipato kimepungua kwa sababu muda huu mtu unajikuta unatumia zile ambazo ulikuwa umeweka kama akiba, lakini kipindi ambacho kulikuwa hakuna ugonjwa, uhakika wa kuingiza ulikuwepo.

 

Kwa hiyo hali hii imeathiri mambo mengi. Lakini kwa upande wangu ninaipongeza Serikali kwa jitihada ambazo zimefanyika na zinazoendelea kufanyika kwa ajili ya kupambana na Corona. Pia sisi tusikilize kile ambacho tunaelekezwa na tukifuate hicho.

 

OVER ZE WEEKEND: Tunajua MwanaFA ni rafiki yako mkubwa sana, ulijisikiaje alipojitangaza kuwa ameathirika na Corona?

AY : MwanaFA ni rafiki yangu na urafiki umepitiliza hadi tumekuwa ndugu sasa, kitu chochote kibaya kitakapompata lazima nijisikie vibaya sana. Niliumia sana na kila wakati nilikuwa nampigia simu kujua anaendeleaje hadi pale alipopata nafuu. Sasa hivi anaendelea vizuri.

 

OVER ZE WEEKEND: Kwa kipindi hiki cha Corona unafanya nini?

AY: Kama unavyojua, sasa hivi hatutoki nyumbani labda niwe na kitu kikubwa cha kufanya. Kwa hiyo nipo tu nyumbani nafanya mazoezi ya viungo, kuimba na kazi ndogondogo za nyumbani, lazima niwasaidie waliopo nyumbani pia.

 

OVER ZE WEEKEND: Kumekuwa na tetesi za hapa na pale mitandaoni kuwa umeachana na mke wako, hii imekaaje?

AY: Sijaachana na mke wangu, lakini si unajua siku hizi mitandao ndiyo kila kitu! Utakuta mtu amesikia jambo fulani, hata kama hana uhakika, anaanza kulisambaza. Mimi nipo na mke wangu na maisha yanaendelea kama zamani.

 

OVER ZE WEEKEND: Sasa hivi uko Bongo, lakini tunajua unaishi pia Marekani na kule bado Corona inashika kasi, sasa nyumba umemwachia nani?

AY: Nimeacha watu kwa kuwa kule kuna watu huwa naishi nao na huwa wananisaidia kuiangalia nyumba nikiwa sipo na ninawaamini. Hata nikikaa nje ya pale kipindi kirefu, nakuta mazingira yako vizuri na hakuna shida yoyote.

 

OVER ZE WEEKEND: Una plani ya kuacha muziki?

AY: Plani hiyo sina na ningekuwa nayo ningeshaacha kabisa. Hata kama nina mambo yangu mengine yanayoniingizia kipato, lakini siwezi kuacha muziki kwa sababu nimetoka nao mbali na upo kwenye damu. Mara nyingi huwa nakaa nafikiri tu kwamba sasa hivi nitoke vipi ili kuweza kuwapa mashabiki wangu kitu roho inapenda.

 

OVER ZE WEEKEND: Una nini cha kuwaambia mashabiki wa Muziki wa AY?

AY: Nina ngoma nyingine naziandaa, hivyo wakae mkao wa kula. Nitakuwa naachia ngoma mara kwa mara. Cha msingi waendelee kunisapoti kupitia chaneli yangu ya YouTube na watazame ngoma zangu mle zipo kibao.

MAKALA: NEEMA ADRIAN

Leave A Reply