Azam FC: Hatutoki Mikono Mitupu Msimu Huu
UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kwamba msimu huu wa 2020/21 hawatatoka mikono mitupu, watapambana kutwaa taji lolote lile katika mashindano makubwa ambayo wanashiriki.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu George Lwandamina, msimu uliopita wa 2019/20 kilikamilisha bila taji kwenye kabati lao ambapo hata lile la Mapinduzi walipokwa na Mtibwa Sugar iliyoinyoosha Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema kuwa msimu huu wapo kipekee na wamejipanga katika kila idara kuhakikisha kwamba wanapata taji.
“Hamna namna lazima tuondoke na taji moja katika mashindano yote makubwa ambayo tunashiriki na ikiwezekana yote kwani uwezo tunao.
“Hapa nazungumzia taji la Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu Bara, ukiangalia kwa namna ambavyo tunafanya kuna jambo letu ambalo tunahitaji kukamilisha, mashabiki watupe sapoti,” alisema Thabith.
Kwenye Kombe la Shirikisho, Azam FC imetinga hatua ya robo fainali baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania huku kwenye ligi ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza mechi 28.
JOEL THOMAS,
Dar es Salaam