The House of Favourite Newspapers

Azam Fc: Kujiwekea Malengo Ya Mataji Ni Kujitesa

0

WAZEE wa kimyakimya, mabosi kutoka Azam FC wameweka wazi kuwa msimu mpya mambo yatakuwa tofauti kutokana na usajili waliofanya pamoja na malengo ya kuwa bora zaidi ya msimu uliopita.

 

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2020/21 Azam FC ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu na haikuweza kupata taji hata moja kibindoni, Championi Jumatatu limezungumza na Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit, ‘Zakazakazi’ ambaye alifunguka mambo mengi namna hii:-

 

Kwenye ligi msimu ujao tunakwenda kutafuta matokeo bora zaidi ya matokeo ambayo tumeyapata msimu uliopita ukilinganisha tangu tumekuwa mabingwa 2013/14, hatujaweza kuwa mabingwa tena lakini kuwa bingwa siyo kitu pekee ambacho tunakihitaji.

 

“Sisi tunahitaji kupiga hatua kubwa kuliko tuliyopita. Kwa mfano msimu uliopita tulimaliza tukiwa nafasi ya tatu, sasa nafasi ya tatu peke yake haitoi picha halisi ila inabidi tuangalie tulimaliza na alama ngapi?

 

“Hizo alama tunapaswa kuzilinganisha na msimu unaofuata kisha hapo tunaweza tukajua kwamba kweli tumefeli. Kwa sababu unaweza kupata alama nyingi msimu huu ila msimu uliopita ukawa umemaliza katika nafasi ya juu.

 

“Hiyo isikuchanganye zaidi unaweza kuwa kwenye nafasi tofauti na msimu uliopita ila wapinzani wako wakawa walikuwa bora kuliko wewe. Kitu kikubwa ni alama ngapi umepata kama alama umepata nyingi kuliko msimu uliopita hiyo ni hatua inayotafutwa na sisi hicho ndicho ambacho tunatafuta.

 

“ Tunahitaji alama nyingi kuliko za msimu halafu mwisho wa msimu tuangalie hizo alama zina maana gani, kama hizo alama zitakuwa zina maana ya ubingwa basi itakuwa ni kwa ajili ya ubingwa na kama tutakuwa tumepata alama nyingi ila tumekosa ubingwa basi lakini tumepiga hatua hilo ni jambo zuri na lipo kwenye mipango yetu.

 

Mkwakwani ugumu upo wapi?

“Mkwakwani ni moja kati ya viwanja vigumu sana siyo kwa kupata matokeo tu bali hata kucheza, unajua sisi tunafanyia mazoezi kwenye uwanja mzuri kila siku unapokwenda kwenye uwanja wako kuna mambo yanakataa na wao wameuzoea.

 

“Ila hicho kitu tunaweka pembeni kwa sababu timu kubwa inapaswa kutafuta matokeo katika uwanja wowote. Lengo la sisi kuwa katika kile ambacho tunakitafuta msimu huu lazima tupate matokeo na lazima tuende katika mazingira hayo kwa kuwa asilimia 50 ya viwanja vya Tanzania vipo namna hiyo. Septemba 27 tutaanza na Coastal Union.

 

Mnahitaji makombe mangapi kabatini?

“Kujiwekea malengo ya mataji ni kujitesa tu unaweza ukajiona haujapata taji ila ukajihesabia umefeli kumbe uhalisia umefaulu sana kuliko ulivyotarajia.

 

“Sisi tunalenga kupata matokeo bora zaidi. Mfano ligi ya England msimu ambao Liverpool walikosa ubingwa, Liverpool ilizidiwa kama pointi moja na Manchester City ambao walitwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 100.

 

“Ukitoa Manchester City aliyefikisha pointi 100, historia inasema kuwa alikuwa ni Chelsea ambaye alifikisha pointi 95,2005, zaidi ya hapo ilikuwa lazima uwe bingwa lakini bahati mbaya Liverpool ilikosa ubingwa kwa sababu Manchester City walipata pointi nyingi zaidi hivyo hawapaswi kujilaumu.

MECHI ZA DABI JE IPOJE?

“Dabi ni dabi unajua kila timu ina kitu ambacho inatafuta, kuna watu wanatafuta hazi za kuzungumza mtaani. Hizi mechi zote za Dabi yaani KMC, Simba, Yanga zitakuwa mechi ngumu sana kwa kuwa kila timu inahitaji ushindi.

“Ninadhani hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwa sababu ni mechi ambazo huwa zinaamuliwa kwa vitu vidogo sana labda kosa la mwamuzi, kosa la mchezaji lakini haitakuwa mechi ya upande mmoja.

USAJILI WENU JE UTAJIBU?

“Ndiyo tumefanya usajili mzuri na wachezaji wenye uwezo. Keneth Muguna mchezaji mzuri sana na nahodha wa muda mrefu ndani ya Gor Mahia, ana uzoefu, Rodgers Kola, Paul Katema, Idris Mbombo mchezaji mkubwa hawa wote tuliowasajili kama wata click itakuwa ni nzuri sana na tutakuwa na kikosi bora sana.

Mpango wa maboresho benchi la ufundi upoje?

“Mpango wa benchi la ufundi hauazi kwa uongozi bali ni benchi la ufundi wenyewe, wakituambia kwamba wanahitaji kuongeza mtu watasema, ila kwa sasa bado hawajatuambia.

“Uongozi mpango wao unakuja kwenye kulitengeneza benchi kwa maana sasa malengo yetu yamekwama kwenda ama benchi likaamua kutoendelea na sisi hapo uongozi unaamua kutengeneza benchi.

“Tunaanza msimu kwa mechi ambazo tutakuwa ugenini, mashabiki waendelea kuwa nasi, tuanzie pale ambapo tumeishia kwa sababu tumemaliza msimu uliopita vizuri.

“Msimu huu ni kimyakimya, wacha miguu ya wachezaji iongee sisi kazi yetu itakuwa ni kuongelea maendeleo ya timu sio mambo yaliyopo nje ya uwanja. Tunasema kimyakimya tusije kuipoteza timu yetu,” anamaliza Zakaria.

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam

Leave A Reply