Makala: Phillip Nkini, Gazeti la Championi Ijumaa, Desemba 30, 2016
TAARIFA kwamba Azam FC wamewatimua makocha wao raia wa Hispania wala hazikunishangaza kwa kuwa kwa mwenendo wa timu yao chini ya Kocha Zeben Hernandez, ulikuwa unaonyesha kuwa lazima jambo hilo litokee.
Ni kweli timu haijafanya vizuri, ni kweli ilikuwa haionyeshi kuwa inaweza kufanya vizuri huko mbeleni na ni ukweli kwamba niliwahi kusema kuwa Azam watawatimua makocha hao muda ukifika.
Halikuwa jambo la ajabu sana kwa kuwa timu ambayo ilikuwa inapewa nafasi ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa sasa ipo katika nafasi ya nne na ikiwa haina matumaini yoyote ya kukwea juu zaidi.
Wapo nyuma ya vinara Simba kwa pointi 14, unataka kuniambia kuwa wanaweza kufanya vizuri na kutwaa ubingwa, sidhani naona kama ni ndoto na wanachokifanya sasa mabosi wa timu hiyo ni kuhakikisha angalau wanarudisha imani kwa mashabiki wao na kumaliza msimu vizuri au kutamba kwenye Kombe la Mapinduzi.
Lakini pia niliposikia kuwa timu hiyo anapewa Kally Ongala lilikuwa jambo zuri kwangu, ingawa wakati huohuo niliitazama Majimaji FC ambayo ilikuwa timu yake kwa jicho lingine.
Majimaji hawakuanza ligi vizuri hadi Ongala alipoichukua timu hiyo na kushinda michezo mitano jambo ambalo linaonyesha ni kocha ambaye alikuwa anaweza kuisaidia timu hiyo kumaliza kwenye nafasi nzuri ya kuwabakiza kwenye ligi.
Kama watakosea kidogo baada ya kocha huyo msomi kuondoka, basi Majimaji watajichimbia kaburi wenyewe na mwisho wa msimu wanaweza kurudi Ligi Daraja la Kwanza walipotoka.
Ongala anakwenda Azam kama mwenyeji, anakwenda akiwa anajua kila kitu kuhusu timu hiyo kwa kuwa ni sehemu ambayo amekaa muda mrefu zaidi akiwa mchezaji na kocha, anajua soka la Tanzania hali ambayo inaonyesha kuwa anaweza kufanya vizuri na timu hiyo.
Jambo moja ambalo Azam wanatakiwa kulifanya ni kumvumilia ili aonyeshe kile ambacho anaweza kukifanya kwenye timu hiyo, wanatakiwa kuhakikisha wanampa ushirikiano kama wa Zeben na siyo kumuachia mambo mengi na mengine kumfanyia chini ya kiwango kwa kuwa ni amezoeleka.
Jambo moja la kujifunza kwa Azam ni kwamba soka linahitaji uvumilivu, waepuke ujuaji mwingi, kweli timu yao imeweza kuweka heshima lakini siyo kwa kulazimisha kama wanavyofanya sasa.
Achana na hawa Wahispania ambao walikuwa nao, tazama makocha wengine wote ambao wamewatimua kuwa walikuwa ni bora na huko walipo wanaonyesha ubora wao zaidi mfano mzuri ni Stewart Hall ambaye aliondoka hapo akiwa na mafanikio makubwa na mwisho wakamrudisha akawapa tena mafanikio.
Lakini pia Joseph Omog, ambaye kwa sasa yupo Simba, amefanya mambo makubwa sana kwenye timu hiyo, ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kama sasa wangemvumilia na kumpa ushirikiano leo hakuna ambaye angekuwa na shaka kuwa Azam wanaweza kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Lakini kama watakuwa wamempa na Ongala timu wakiamini kuwa anaweza kufanya mambo haraka haraka bila kuwa na uvumilivu basi watakuwa wanaitafuta pepo kabla ya kufa.
Soka ni maandalizi, hakuna mafanikio ya soka bila maandalizi Azam wanatakiwa kumpa ushirikiano Ongala na kocha mwingine yeyote lakini wakijua kuwa ana kazi ya kutengeneza timu yao upya na siyo kutwaa ubingwa.
Comments are closed.