Kampuni ya Azam Media Ltd, imebaini vipande vya picha jongefu vinavyosambaa kupitia mitandao ya kijamii vikimuonesha mwigizaji na mtengeneza filamu, Deogratius Shija, akiwatuhunu baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yetu kwa vitendo vya rushwa.
Kampuni yetu inamuarifu Shija na umma kwa ujumla kuwa, haivumilii vitendo vya rushwa, udanganyifu na mbinu zozote chafu katika kusaili maudhui kwa ajili ya kuonyeshwa katika chaneli zetu, kadhalika hatupendezwi na tabia ya watengeneza maudhui kutunga shutuma dhidi ya watendaji wetu kwa sababu tu kazi zao hazikupitia kwenye chujio la kupima ubora.
Kwasababu hizo, tunatoa muda wa wiki mbili kwa Deogratias Shija, kuwasilisha ushahidi au vielelezo kuhusu tuhuma alizozitoa kwa Mkurugenzi Mtendaji au kwenye mamlaka za kisheria, TAKUKURU, Film Board, au Jeshi la Polisi, ili kuwezesha hatua stahiki zichukuliwe kwa watuhumiwa wote wanaodaiwa kuihujumu kampuni kwa vitendo vyote kinyume na taratibu za kazi.
Kampuni yetu ina utaratibu maalum wa ndani, ulio wazi na shirikishi katika manunuzi ya filamu na maudhui mengine kutoka kwa wazalishaji binafsi.
Azam Media Ltd inatumia fursa hii kuwaomba wadau wa filamu nchini kufuata njia sahihi zinazokubalika kisheria ikiwemo kutoa taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Filamu, Polisi au TAKUKURU pale wanapokuwa na ushahidi wa madai yao badala ya kutumia njia ambazo zinaweza kuleta taharuki na taswira mbaya kwa jamii ndani na nje ya Tanzania.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano kwa Umma
1.12.2023