The House of Favourite Newspapers

Azinduka baada ya kupoteza fahamu miaka 27!

 

MWANAMKE mmoja kutoka Umoja wa falme za Kiarabu (UAE) aliumia katika ajali ya gari iliyotokea mwaka 1991 na kupoteza fahamu lakini sasa amewastaajabisha wat wengi baada ya kuzinduka kutoka kwenye koma iliyomchukua miaka 27 akiwa amepona.

 

Munira Abdulla alipata ajali akiwa na umri wa miaka 32 na kupata jeraha katika ubongo, ilikuwa ni ajali ya kugongwa na basi wakati akiwa anaelekea kumchukua mtoto wake shuleni.

 

Mtoto wake Omar Webair, alikuwa na umri wa miaka minne wakati yeye na mama yake walipopata ajali. Katika ajali hiyo Omar ambaye alikuwa ameketi katika kiti cha nyuma hakujeruhiwa hata kidogo na alikutwa akiwa amekumbatiwa na mama yake.

 

Bi. Abdulla alijeruhiwa vibaya lakini mwaka jana akiwa hospital moja Ujerumani alianza kurudisha fahamu. Omar amesimulia  kuhusu ajali waliyoipata na kuelezea utaratibu wa matibabu ya mama yake yaliyochukua miaka mingi.

 

“Sikuwahi kukata tamaa kwa sababu kila siku nilihisi kuwa kuna siku mama yangu ataweza kuamka,” Omar anaeleza.

 

Omar aliongeza kusema kuwa sababu kubwa ambayo imemfanya asimulie mkasa uliomkuta mama yake ni kutaka kuwaambia watu kuacha kukata tamaa kwa watu wanaowapenda na mtu akifikia hatua hiyo haimaanishi kuwa amekufa.

 

 

Mama mkwe wa Munira ndiye alikuwa dereva.

“Mama yangu alikuwa amekaa na mimi katika kiti cha nyuma  na alipoona tunakaribia kupata ajali, alinikumbatia ili kuniokoa katika ajali hiyo,” anasema Omar.

 

Katika ajali hiyo Omar hakuumia bali alibaki na jeraha dogo kichwani lakini mama yake ambaye aliumia alichelewa kupata matibabu kwa saa kadhaa.

 

Bi. Abdalla alifikishwa hospitali baada ya muda wa saa kadhaa kupita na baadaye alihamishiwa mji wa London ambako  walisema kuwa amepoteza fahamu lakini akiwa ana uwezo wa kuhisi maumivu.

 

Baada ya muda alirudishwa katika mji wa Al Ain katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambako alikuwa akiishi na mtoto wake Omar, na kuendelea kuzunguka katika vituo mbalimbali vya afya kulingana na bima aliyokuwa nayo.

 

Alikuwa anakula kwa mrija na kumfanya aendelee kuishi na mara kwa mara alifanyiwa mazoezi na vipimo vya viungo ili kuhakikisha kuwa misuli yake haidhoofiki kwa kuwa alikuwa hatembei.

 

Mwaka 2017, familia ilipokea msaada wa fedha kutoka serikalini ili kumwezesha Bi. Abdulla kwenda Ujerumani kwa ajili ya matibabu.

 

Alifanyiwa upasuaji mara kadhaa ili kurekebisha mkono wake uliopunguzwa na kuweka sawa misuli ya mguu, na alipewa pia dawa ili kuboresha hali yake, ikiwa ni pamoja na kuamka kwake.

 

Baada ya mwaka mmoja watu walimsikia Omar anajibizana na mama yake ndani ya chumba cha hospitalini, jambo lililoonyesha kwamba alikuwa amezinduka.

 

“Kulikuwa na kutoelewana katika chumba alichokuwa amelazwa na alihisi kuwa niko hatarini, jambo ambalo lilimfanya (mama) ashtuke,” Omar alisema.

 

 

” Alikuwa anahangaika kutoa sauti na nilikuwa nahangaika kuita madaktari ili wampime na walisema kuwa kila kitu kilikuwa sawa.

 

“Siku tatu baadaye, niliamka nikasikia mtu ananiita kwa jina langu. Alikuwa ni yeye, alikuwa anaita jina langu, nilikuwa kama ninapaa kwa furaha.   Kwa miaka mingi nimekuwa nikiota siku hii ifike na jina langu lilikuwa neno la kwanza kulitamka baada ya miaka 27,” Omar alieleza.

 

Na baadaye akawa anaweza kuwasiliana na sasa baada ya maumivu ya muda anaweza kuzungumza. Bi. Abdalla ameweza kurudi Abu Dhabi, ambako anaendelea kupata tiba ya viungo kwa mazoezi na kupata ushauri hasa wa namna ya kukaa na kufanya misuli kuwa imara.

 

Kuna kesi chache sana za watu kupona baada ya kupoteza fahamu kwa miaka mingi na kuendelea kuwa wazima kabisa.

 

Watu ambao wanapata hali hiyo na kurudi kwenye ufahamu wao baada ya koma ya muda mrefu mara nyingi tatizo lao huwa linatokana na madhara katika ubongo.

 

Bingwa wa zamani wa mashindano ya magari duniani, Michael Schumacher aliwahi kupata koma baada ya kupata ajali mwaka 2013 huko Ufaransa. Alipoteza fahamu kwa muda wa miezi sita kabla hajarudishwa kwao Switzerland kuendelea na matibabu.

Comments are closed.