The House of Favourite Newspapers

Baada ya Harmonize Kujitoa… Rayvanny Taa Nyekundu Wasafi

DAR ES SALAAM: UNA kifua nikupe ubuyu? Staa mwenye kiwango cha juu ndani ya Bongo Fleva, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ anayepiga mzigo na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), muda wowote anaweza kuondoka katika familia hiyo inayoongozwa na mnyama mkali, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’. 

 

Mipango ya kumng’oa staa huyo mwenye sifa ya utunzi bora wa mashairi leboni hapo, inasukwa na meneja mmoja maarufu wa wasanii nchini akishirikiana na tajiri mwenye fedha zake.

 

Inaelezwa nia ya kumng’oa Rayvanny kwenye mikono ya Diamond, ni mwendelezo wa kuidhoofisha WCB iliyo chini ya mameneja wenye ujazo wa juu Bongo, Sallam Shariff ‘SK’, Said Fella ‘Mkubwa’ na Hamisi Taletale ‘Babu Tale’.

 

Habari za kuwindwa staa huyo, zimevuja ikiwa ni siku chache tangu staa mwingine kwenye muziki huo, Rajab Abdul ‘Harmonize’ amwage manyanga na kuanza kufanya kazi akiwa na lebo yake ya Konde Gang.

Harmonize ambaye kibao chake ‘Never Give Up’ bado kinafanya vizuri kikifuatiwa na ‘Kwangwaru Remix’ alichoachia hivi karibuni, hivi sasa yupo busy kuhakikisha lebo yake ya Konde Gang inasimama. Yupo chini ya mameneja wenye uwezo mkubwa kwenye tasnia hiyo, akiwemo Sebastian Ndege ‘Jembe ni Jembe’ ambaye ni mmiliki wa kituo kimoja cha redio jijini Mwanza.

HABARI MEZANI

Ubuyu huo umepenyezwa na rafiki wa karibu na meneja ambaye anayesuka mipango ya kumchukua Rayvanny anayesumbua na kibao cha ‘Vumbi’ alichopiga kolabo na Diamond Platnumz. Kizungumza na Amani kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, chanzo hicho kilisema: “Mipango ipo tayari, Rayvanny muda wowote anatoka WCB.”

Chanzo hicho kilitutajia jina la meneja huyo na namba zake za simu, lakini kwa busara za kihabari, kwa sasa tunahifadhi jina lake hadi mzani utakapokuwa sawa. Kinaendelea kufunguka: “Huyo jamaa amefanikiwa kumshawishi tajiri mmoja mkubwa sana ambaye amekubali kuwekeza kwenye muziki wa Rayvanny kwa sababu anaujua uwezo wake.

“Hivi ninavyozungumza na wewe, tayari huyo meneja ameshazungumza na Rayvanny ingawa walichokubaliana mimi hajaniambia, ila amesema mambo ni moto, muda wowote Rayvanny atakuwa chini yake.

“Unajua kaka mjini mipango na watu wanajua kutumia fursa. Jamaa muda mrefu alikuwa akisemasema kuwa Rayvanny ni msanii mzuri na anapanga kufanya naye kazi, lakini alikuwa akihofia ukubwa wa WCB lakini sasa ametumia fursa. “Alivyoona Harmonize ameondoka, akaona kumbe inawezekana. Ndiyo maana akajitosa kuhakikisha anamng’oa. Ni suala la muda tu.”

MENEJA AFUNGUKA

Amani lilifanikiwa kumpata meneja huyo ambaye mwanzo alikuwa hataki kutoa ushirikiano kwa maelezo kuwa bado ni mapema, lakini baadaye alikubali kufunguka. “Na nyie ni wadaku sana bana… jambo la msingi tu mjue ni kweli mchakato wa kumchukua Rayvanny upo, unafanyika na utafanikiwa,” alisema meneja huyo, naye akiomba asiandikwe gazetini kwa kile alichodai kitamkwamisha mipango yake hiyo.

“Yule bwana mdogo ana uwezo mkubwa sana, ndiye mwenye uwezo wa kutunga mashairi makali kuliko msanii mwingine yeyote aliyepo WCB. Anaweza kusimama peke yake, ndiyo maana nimehangaika kupata mtu ambaye amekubali kuwekeza fungu kwa ajili ya kumsaidia.

“Naijua nguvu ya Rayvanny. Kwangu namuona ni mkubwa kuliko hata Harmonize. Ni suala la kupata menejimenti nzuri, ambayo ni mimi na mwenzangu,” alisema. Alipoulizwa kama ameshafanikiwa kukutana na Rayvanny na kuzungumzia naye suala hilo, alisema kwa sasa anaomba jambo hilo liwe kwenye mabano.

“Leave it in the brackets (acha hilo likae kwenye mabano), nikisema sana nitaharibu mambo. Elewa kuwa mambo mazuri yanakuja na Rayvanny atakuwa chini ya lebo nyingine kubwa zaidi ambayo itakuwa na ushindani mkubwa kwenye Bongo Fleva,” alisisitiza na kuongeza:

“Itatingisha na watu hawataamini. Tumedhamiria kufanya mapinduzi makubwa kwenye Bongo Fleva. Ni suala la muda tu. Watu wavute subira.”

RAYVANNY ASAKWA

Amani lilimsaka Rayvanny juzi Jumanne ili aeleze kama alishakutana na meneja huyo au lah bila mafanikio; awali simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa, baadaye haikupatikana tena. Juhudi zaidi za kumtafuta zinaendelea na tutawaletea maelezo yake pindi atakapopatikan

Comments are closed.