The House of Favourite Newspapers

Baada ya kipigo, Kerr aibuka, atoa masharti magumu

0

kocha

Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr.

Omary Mdose, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, amekanusha habari zilizoenea kwamba yupo katika harakati za kutimuliwa akisema ni za uzushi lakini amekuja na mbinu ambayo hata hivyo inaonekana ni masharti magumu kwa wachezaji.

Muingereza huyo amedai kwamba wachezaji wake kwenye mechi wamekuwa hawafanyi kile anachowafundisha mazoezini, lakini amewataka mpaka msimu huu unamalizika Mei 7, mwakani, basi wawe wamefunga mabao si chini ya 100, kitu ambacho inaonekana hakiwezekani kwenye Ligi ya Bongo.

Mpaka sasa kikosi cha Simba kimefunga mabao nane katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara kwa kukusanya pointi 15 kibindoni na kinashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo ambapo kati ya mabao hayo, Mganda, Hamis Kiiza, amefunga matano.

Kerr ambaye alitua nchini mwishoni mwa Juni, mwaka huu, ameliambia gazeti hili kuwa anapenda kuona kila straika aliyepo kikosini hapo akifunga mabao si chini ya kumi huku akiwataka na viungo nao kufanya kazi ya kufunga kama ilivyo kwa viungo wengine duniani.

Kocha huyo ambaye ni shabiki mkubwa wa Manchester United ya England, aliongeza kuwa ukiangalia katika kikosi chake utagundua kwamba wanao uwezo wa kutengeneza nafasi si chini ya nne za kufunga mabao ambapo kama wakiwa makini basi lengo la kufikisha mabao hayo litatimia.

“Katika kila mchezo tunao uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga mabao kuanzia nne kwenda mbele, lakini utashangaa tunapata ushindi kiduchu au kufungwa kabisa, tatizo ni umakini kwa wachezaji lakini kama umakini ukiwepo basi uwezo wa kuibuka na ushindi mnono kwenye mechi zetu zote ni wa hali ya juu.

“Litakuwa jambo jema kama tukimaliza msimu huu kwa kufunga mabao 100, najua hilo linawezakana kwani kila kitu ni malengo, japo miundombinu ya viwanja ni kikwazo kikubwa,” alisema Kerr ambaye hivi karibuni kumekuwa na tetesi za kutimuliwa kuinoa timu hiyo.

Leave A Reply