BAADA YA KUACHWA NA MUME WAGANGA WA MFILISI MKE!

DAR ES SALAAM: Historia ya maisha ya Aisha Said mkazi wa Gezaulole Kigamboni jijini Dar es Salaam baada ya kuachwa na mumewe inasikitisha. 

 

Jumatatu wiki hii Amani lilimtembelea Aisha nyumbani kwake na kushuhudia akiishi maisha duni yeye na wanawe watano huku habari zikieleza kuwa, enzi zake alikuwa ‘mambo safi’ kimaisha.

 

AMEYAFIKIAJE MAISHA DUNI?

Waganga mbalimbali wa kienyeji wanatajwa kumfilisi huku tiba ya ugonjwa wa mtoto wake aitwaye Hassan Juma ikitajwa kuwa chanzo cha majanga yote. Ukimuona mtu mzima analia ujue lipo jambo zito na ndivyo ilivyo kwa Aisha ambaye anaanza simulizi yake iliyoambatana na machozi kama ifuatavyo: “Mwanangu alipata tatizo la kupooza akiwa shule ya msingi, (Hakumbuki mwaka) darasa la saba.

 

“Akiwa katika hali hiyo alifaulu kwa kupata alama ‘A’ na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini alishindwa kuendelea kutokana ugonjwa alioupata. ”Hali hiyo liniuma sana, nikaamua kuanza kupigania afya ya mwanangu ili aweze kutimiza ndoto zake.”

 

MGANGA WA JADI AIBUKA

Aisha akiwa katika harakati za kumtibia mwanaye kwenye hospitali mbalimbali jijini Dar  ikiwemo Muhimbili na CCBRT bila mafanikio, ghafla aliibuka mganga mmoja wa kienyeji (jina linahifadhiwa) na kujitapa kwamba tatizo la Hassan ni ndogo kwake. “Alinipigia simu na kuniambia kuwa yeye anaishi Mombasa (Kenya) na kwamba ameona mwanangu anavyoteseka akasema anaweza kumtibu.

 

“Alinipa maneno mengi ya matumaini; nikamwamini akaniambia nitafute kiasi cha shilingi laki sita (600,000) mwanangu atapona bila wasiwasi,” alisema Aisha ambaye hakujua hata namba yake ya simu mganga huyo aliipataje? Baada ya maelezo ya mganga, mama huyo aliyekuwa na shauku kubwa la kuona mwanaye anapona alianza kutimiza masharti ya mganga huyo likiwemo la kutafuta kiasi cha fedha alichoambiwa.

 

SAFARI YA MOMBASA

Aisha hakuchelewa kutimiza aliyoambiwa na mganga kwani alikuwa akijimudu kifedha kutokana na kipato alichokuwa akipata katika biashara yake ya duka la bidhaa mbalimbali alilokuwa akilimiki eneo la Msasani. Kutokana na hilo, mganga wake alimwambia anatakiwa amchukue mgonjwa wake haraka hadi mkoani Tanga na baadaye kusafiri hadi Mombasa ambako ugonjwa wa Hassan ungekwenda kutoweshwa.

 

Baada ya kukutana Tanga pembezoni mwa bahari, Aisha, mwanaye na mganga wao walivuka upande wa Mombasa hadi kwenye kichaka ambapo mganga alisema hapo ndiyo ‘kilingeni’ ambako ndumba zingefanyika. Wakiwa hapo kichakani mtaalamu huyo alichimba shimo la futi takriban saba na kumfukia Hassan kisha kumuacha wazi eneo la kifua kuja kichwani huku mwili mwingine ukiwa ardhini.

 

Muda aliotakiwa Hassan kufukiwa na kukaa ardhini akiwa hai katika hali hiyo ni saa 12; marufuku ya kula chochote iliwekwa juu yake na kwamba alichotakiwa kunywa ni dawa tu aliyopewa na mganga. Mbwembwe zote za matibabu ya mganga zilipokamilika Aisha aliambiwa arudi nyumbani huku akiahidiwa afya ya mwanaye ingetengemaa ndani ya muda mfupi.

 

Hata hivyo, haikuwa kama alivyoambiwa, fedha aliyotoa ilikuwa imechukuliwa na mgonjwa hakuwa na nafuu yoyote. Mara kadhaa mganga alipoulizwa alisema: “Ugonjwa huingia haraka lakini hutoka taratiba.” Jambo lililomfanya ageuzegeuze tiba zake kila mara huku akiendelea kumpiga Aisha fedha kama atakavyo.

 

AISHA AFILISIKA

Kutokana na janjajanja ya mganga huyo Aisha alijikuta akitumia fedha nyingi ambazo zilisababisha duka lake kufa na maisha kuanza kwenda hali jojo. Aisha alikiri kuwa hata baada ya kulizwa fedha nyingi na mganga huyo kutoka Mombasa aliendelea kusaka tiba kwa waganga wengine ambao ni kama walikuja kupigilia tu msumari wa mwisho wa kumfilisi fedha bila mwanaye kupona.

 

“Nilipokosa fedha nikaanza kuuza vitu vyangu vya ndani, nikamaliza vyote, isitoshe nilikuwa nafuga kuku lakini nazo zimeishia kwa waganga, mara waniambie nipeleke vitu fulani yaani ilmradi ni kunichukulia vyangu na wao wavitumie,” alisema Aisha huku akimwaga machozi.

 

AANZA KAZI YA KUPONDA

MAWE Baada ya mikasa yote ya kutapeliwa na waganga wa kienyeji ambao hatimaye walitokomea, Aisha alijikuta katika wakati mgumu wa kulea watoto wake watano alioachiwa na mumewe ambao wanaonekana pichani ukurasa wa mbele. Kufuatia ugumu huo wa maisha alilazimika kufanya kazi ya kuponda mawe na kuuza huku akiwa anatunzwa kwenye kibanda alichopewa na msamaria mwema.

 

Amani ambalo lilifika katika kibanda hicho lilishuhudia maisha ya mateso juu ya mateso ya watoto hao wanaokabiliwa na shida ya chakula, mavazi na malazi huku Hassan ambaye ni mgonjwa hali yake ikisikitisha zaidi. Aisha anawaomba wasamaria wema wamsaidie aweze kufungua hata genge ili aweze kuendelea kuwalea wanaye.

 

OMBI LA AMANI

Dawati la Amani linawaomba wananchi kuwa makini na baadhi ya waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakitumia ulaghai kuwaibia watu hasa wenye matatizo kama Aisha ambaye mwanzo alikuwa amepanga nyumba nzima, anamiliki duka, anakula anachotaka na wanaye lakini leo amebaki mikono mitupu.

Waandishi: Zaina Malogo na Richard Bukos.

Toa comment