BAADA YA KUCHUNGULIA KIFO, HII NDIYO SIMULIZI MPYA MAISHA YA HAWA

Msanii wa Bongo Fleva, Hawa Said ‘Hawa Nitarejea’.

AMA kweli Mungu hamtupi mja wake! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kusikia habari njema za afya ya msanii wa Bongo Fleva, Hawa Said ‘Hawa Nitarejea’.

 

Afya ya Hawa kwa sasa imeimarika na kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kuchungulia kaburi, jambo ambalo hata yeye mwenyewe hakulitegemea kwani alishakata tamaa ya kuishi. Mwishoni mwa mwaka jana, Hawa alipelekwa kwenye matibabu nchini India kutokana na tatizo lake la tumbo kujaa maji.

 

Jitihada hizo za matibabu ya Hawa zilifanywa na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyeshirikiana naye kwenye Wimbo wa Nitarejea. Baada ya kurejea Bongo, Hawa aliwekwa mafichoni kwenye hoteli moja jijini Dar kutokana na maelekezo kutoka kwa madaktari ambao walitaka iwe hivyo kwa miezi mitatu.

 

Baada ya miezi hiyo mitatu, Hawa alirejea nyumbani kwao, Buguruni-Rozana jijini Dar kuendelea na maisha yake kama kawaida. Risasi Mchanganyiko lilimuibukia nyumbani hapo ili kufanya naye mahojiano kuhusu hali yake kwa sasa na mambo aliyoyapitia.

“Kwa kweli ninamshukuru sana Mungu maana bila yeye, huenda nisingekuwepo, leo hii naweka tabasamu usoni, lakini niliteseka mimi jamani. Hadi ninasafiri kwenda India nilikuwa na maumivu makali hadi nilihisi kama nataka kuchanganyikiwa, yaani hadi kumsimulia mtu nahisi kama nitampunja kwa sababu hayaelezeki, yalikuwa makali sana.

 

“Kwanza tumefika kule (India), wiki nzima nilikuwa ninafanyiwa vipimo tu. Mara leo naingizwa kwenye mashine nachekiwa mwili mzima, siku nyingine naminywa tumbo. Hadi ninaingizwa kwenye operesheni nilikuwa naona kama naenda kufa ingawa madaktari walinihakikishia kuwa uwezekano wa kupona ni asilimia 95, ila niliona kama wananifariji tu ili nisiogope.

 

“Nilikaa chumba cha upasuaji kwa saa zisizopungua sita huku madaktari wakihangaika na mimi, wakati huo mama yangu alikuwa nje ya wodi analia, alikuwa anajua ninakufa (analia) ila kumbe siku yangu haikufika, nikatoka kwenye chumba cha upasuaji salama kabisa.

 

“Ila baada ya ganzi kuisha nilihisi maumivu ambayo sijawahi kuyahisi, halafu hali nilihisi kuwa mbaya zaidi pale ambapo walinitoa mashine ya kupumulia, nilianza kutapatapa nikawa ninashindwa kupumua mwenyewe kwa sababu nilishazoea kupumulia gesi, lakini wakaniambia inabidi nifanye mazoezi ili nizoee kupumua mwenyewe. Nilikuwa siwezi hata kuongea, nilikuwa kama mtoto, yaani kama kitu sitaki nalia tu maana nikiongea hata maneno mawili tu pumzi inakata.

“Kuna wakati nilihisi kama mwili siyo wangu, yaani kama umeoza hadi nikamwambia mama yangu mbona kama ninakufa sitarudi tena nyumbani kama mambo yenyewe ndiyo haya maana nilipasuliwa katikati ya matiti.

 

“Nilikuwa siwezi kuinuka ni kulala chali tu, sigeuki kushoto wala kulia, mgongo ulikuwa unauma, kuna wakati nilitamani kujinyoosha, lakini naambiwa nitulie dawa iingie. Nilikuwa nakula kwa shida sana, sikuwa nahisi ladha ya kitu chochote, lakini sasa hivi nakula vizuri, niko fiti kabisa, sisikii maumivu yoyote ingawa kuna baadhi ya dawa naendelea kuzitumia,” alisema Hawa.

 

KUHUSU KURUDI KWENYE MUZIKI

Hawa alisema kwa sasa hawezi kutoa jibu la moja kwa moja kwa sababu anataka ajitafakari ili akiamua kuingia kwenye muziki, aingie jumlajumla. “Siwezi kusema nitarudi lini kwenye muziki kwa sababu ni uamuzi mgumu, siyo wa kukurupuka, sasa hivi naogopa sana, nisije kurudia ya mwanzo kwa sababu awali ilikuwa ni msongo wa mawazo.

 

Nikiingia kwenye muziki halafu mambo yakibuma, nitapata tena mawazo ila muziki naupenda sana. “Siwezi kuacha muziki, lakini kwa sasa ninajitafakari nirudi kwa namna gani, natuliza akili kwanza,” alisema Hawa.

KUHUSU KUJIUNGA NA WCB

“Kuhusu kujiunga WCB (Lebo ya Wasafi Classic Baby), Diamond akiamua wala sitapinga hilo ila siwezi kujiwekea matamanio kwenye moyo wangu kwa sababu itanigharimu, nikitamani halafu isipokuwa hivyo yatatokea yaleyale, kwa hiyo vyovyote itavyokuwa basi itakuwa kheri tu,” alisema msanii huyo.

 

AFUNGUKA KUPANGISHIWA NA DIAMOND

“Juu ya kupangishiwa sehemu ya kuishi, ni kweli Diamond alinipangishia sehemu ya kukaa yenye utulivu nipumzike kama ambavyo madaktari walishauri, lakini siwezi nikasema ni wapi ila ni pazuri, nimekula raha ambayo sijawahi kula tangu nizaliwe, yaani Mungu ambariki yule kaka (Diamond),” alimalizia Hawa ambaye kwa sasa yupo fiti kabisa.

Stori: SHAMUMA AWADHI, RISASI MCHANGANYIKO

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment