The House of Favourite Newspapers

Baada Ya Kufeli Msimu Huu… Usajili Mpya Simba Kufuru Kuitikisa Afrika

0

BAADA ya kushindwa kufikia malengo yao msimu huu, uongozi wa Simba umeibuka na kuchimba mkwara mzito kuwa mapema tu tayari wameanza mipango ya kurejesha utawala wao msimu ujao kwa kufanya usajili mkubwa wa kuitikisa Afrika.

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kutangazwa rasmi kufunguliwa kwa dirisha la usajili, Simba katika maboresho ya kikosi chao wamehusishwa na majina makubwa yakiwemo straika wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini Ranga Chivaviro, winga wa AS Vita, Erick Kabwe pamoja na beki wa Ihefu, Yahya Mbegu.

Simba ambao jana Ijumaa usiku walishuka uwanjani kuvaana na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, msimu huu walikuwa na malengo ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo yote yanaonekana kushindikana.

Akizungumzia mipango yao kuelekea msimu mpya wa 2023/24, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema: “Kwanza kabisa ningependa kuchukua nafasi hii kwa niaba ya uongozi kuwaomba radhi wanachama, mashabiki na wadau wa Simba kwa kuwa na msimu mbaya kwa mara ya pili mfululizo. Kimsingi hakuna sababu ya kumtafuta mchawi kwa kuwa kila mmoja amehusika na kuumizwa na kilichotokea.

“Jambo la msingi ni kuwa tumechukua kilichotokea kama changamoto na kufanya tathmini ya wapi tumekosea na tunatarajia kufanya maboresho makubwa ya kikosi chetu, tunasubiri ripoti ya benchi la ufundi kujua ni mchezaji gani atakuwa sehemu ya mahitaji kwa msimu ujao na yupi atalazimika kuondoka.

“Lakini tumepanga kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya pamoja na mipango ya kambi bora ya kabla ya msimu kuhakikisha tunarejesha utawala wetu msimu ujao.”

Leave A Reply